Na Mwandishi Wetu-Dodoma
KATIBU Mtendaji wa Chama cha ADA-Tadea, John Shibuda, amewataka wanasiasa na viongozi wastaafu wa Serikali kuacha tabia ya kujenga dhana inayokuza mpasuko kwa jamii kwa kuwa makini na kauli zao.
Hayo aliyasema mjini hapa jana kutokana na kauli ya Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowassa ya kuwatetea masheikh wa Jumuiya ya Mihadhara (Umasho) kuwekwa mahabusu kwa miaka kadhaa bila kesi yake kuamuliwa kuwa uonevu.
Shibuda alidai kauli ya Lowassa imekosa umakini na kutozifanya hoja zake zikose uhalali .
“Wanasiasa ni vema wajenge fikra na kauli zenye umakini, hekima na mafunzo ya utetezi wa haki kwa kufuata usawa bila ya kuongeza chumvi au shinikizo la mgawanyiko katika jamii.
“Masuala yanayobeba tuhuma za uhalifu au jinai ni vema vyombo husika vikapewa nafasi ili kujitosheleza na kujiridhisha katika taaluma,” alisema.
Shibuda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini, alisema katika hoja iliyoibuliwa na Lowasa kuhusu waislamu, mtu mwenye weledi na umakini itawia vigumu kubaini maono yake, shabaha na kusudio lenye msingi dhidi ya madai hayo kwa sababu ni vigumu mtu mmoja kusafiria farasi wawili kwa wakati mmoja.
“Dira ya siasa ilenge katika kuleta mapinduzi ya fikra na uchumi kwa kuzingatia matumizi salama ya matamshi, mipaka ya utawala iwe na rutuba ya kuhami rasilimali jamii inufaike.