30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SHERIA YAJA KUZIBANA NGO’S

Na FREDY AZZAH-DODOMA

MUSWADA wa Sheria ya Fedha wa 2017 uliowasilishwa bungeni hivi karibuni umezitega Taasisi zisizo za Serikali (NGOs) na sasa umependekeza hesabu zake ziwe zinakaguliwa ili zilipe kodi pindi zinapopata faida.

Pia muswada huo umetoa ufafanuzi kuwa nyumba zisizothaminishwa zinazotakiwa kulipiwa Sh 10,000 za kawaida na Sh 50,000 kwa ghorofa kwa mwaka ni zile za mijini tu.

Sehemu ya tatu ya muswada huo, inapendekeza marekebisho ya sheria ya kodi ya mapato, sura 332, inayotaka kufanya marekebisho ya kifungu cha tatu kufuta baadhi ya maneno katika tafsiri ya maneno biashara, leseni na mfuko wa ukarabati.

“Marekebisho haya yanapendekezwa ili kutoa nafasi kwa taasisi zinazofanya shughuli zake kwa kutopata faida, kuthibitisha kwa kupitia taratibu za kawaida za kodi badala ya kuwaondoa katika utaratibu huo.

“Kifungu cha 19 kinapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 19(2)(d) kwa ajili ya kuondoa utata wa kisheria na kupungua kwa mapato kutokana na zuio au makubaliano ya matarajio ya kifedha kwa kufanya miamala iliyowekwa kama biashara nyingine na kuzuia mapato yaliyopatikana.

“Aidha kifungu cha 64 kinapendekeza marekebisho kwa madhumuni ya kutoza kodi kwenye taasisi za kujitolea. Dhumuni la hatua hii ni kuondoa utata na kuongeza uhakiki ili kuzifanya taasisi zinazostahili punguzo la kodi kueleweka wazi,” inasema sehemu ya muswada huo.

Pia katika sehemu ya tisa, muswada huo unapendekeza kuifanyia marekebisho sheria ya kodi za majengo ya mamlaka ya miji ili kumpa mamlaka Wazari wa Fedha kutoza kodi ya majengo kwa nyumba zote zilizopo mijini.

Marekebisho hayo yanapendeza kubainisha kiwango cha tozo kwa nyumba ambazo hazijafanyiwa uthamini kwa mujibu wa sheria ya kodi za majengo ya mamlaka.

Sehemu ya nne ya muswada inapendekeza kuifanyia Marekebisho Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, (Sura ya 290) ambapo kifungu cha 31 A, kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kuiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya ushuru wa mabango ya matangazo kwa nchi nzima.

“Kifungu cha 37 kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kuwatambua wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara katika maeneo yasiyo rasmi.

“Aidha kifungu cha 67 cha Sheria kinapendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa kukifuta na kukiandika upya ili kuongeza adhabu inayotolewa kwa mtu anayekiuka masharti ya sheria na ambapo hakuna adhabu iliyobainishwa na kuwa faini isiyopungua shilingi 200,000 na isiyozidi shilingi milioni moja au kifungo kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja na kisichozidi miaka miwili,” unasema muswada huo.

Pia unapendekeza kifungu cha 69 kirekebishwe ili kuwezesha dhana ya malipo ya bima yaliyolipwa nje ya nchi yanalipiwa kodi hapa nchini.

“Kifungu kipya cha 83B kinaongezwa ili kuweka kodi ya zuio kwenye mauzo ya madini yanayouzwa na wachimbaji wadogo na wa kati.

Sehemu ya tano inapendekeza kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 18 cha Sheria ya Madini, Sura ya 123, ili kuzuia uuzaji wa madini nchi za nje.

“Sehemu hii inapendekeza kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 90 ili kuweka ada ya ukaguzi kwenye madini yatakayouzwa nje ya nchi na kiwango kinachopendekezwa ni asilimia moja ya thamani ya madini husika kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

“Sehemu hii pia inapendekeza kufanya marekebisho kwenye kifungu cha 112 cha Sheria ya Madini, ili kumpa waziri anayehusika na madini kutengeneza kanuni za kuwezesha ukaguzi wa madini na utozaji wa ada ya ukaguzi kwa yatakayosafirishwa nje ya nchi,” ulisema muswada huo.

Sehemu ya Sita inapendekeza marekebisho ya Sheria ya Fedha, sura 348 kwa kuongeza kifungu cha 6A ili kuweka sharti kwa Wizara na Taasisi za Serikali kukusanya mapato yote kupitia mfumo wa ukusanyaji mapato uitwao ‘Government e-Payment Gateway System (GePG)’.

Pia unasema lengo la hatua hiyo ni kuzuia uvujaji wa mapato na kuimarisha ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi.

Sehemu ya Saba ya Muswada inapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya TRA Sura ya 399.

Sehemu ya Nane ya Muswada inapendekeza kurekebisha Sheria ya Usimamizi wa Kodi Sura ya 438.

“Marekebisho haya yanalenga kuboresha mwitikio wa hiari wa ulipaji kodi kwa wakati kupitia uboreshaji wa taratibu za utozaji riba kwa malipo ya kodi anayechelewa kulipa kwa wakati, kuwezesha TRA kukusanya malipo ya faini yatokanayo na adhabu kwa kukiuka sheria za kodi kama ilivyokusudiwa na sheria hizo.

“Aidha, lengo la mapendekezo haya pia ni kuboresha uwezo wa TRA wa upekuzi na upelelezi wa makosa yatokanayo na sheria za kodi pamoja na kuboresha uwezo wa mamlaka wa kudhibiti makosa dhidi ya sheria za kodi, ikiwamo makosa dhidi ya taratibu za matumizi ya mashine za kielektroniki za ulipaji kodi (EFD’s).

“Kuweka kikomo cha muda wa maombi ya kudai marejesho ya kodi (tax refunds) kwa walipa kodi na kutambua rasmi notisi za madai ya kodi ya majengo (demand notes) zitolewazo na TRA kama ni makadirio ya kodi husika, pamoja na kuhakikisha usahihi na uwazi wa sheria za kodi kwa kufanya marekebisho ya makosa ya kiuandishi yaliyopo katika sheria mbalimbali za kodi,” ulisema mswada huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles