23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Sheria ya Vyama vya Siasa yapingwa mahakama ya Afrika Mashariki

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

VYAMA nane vimefungua kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ), kupinga Sheria ya Vyama vya Siasa iliyoanza kutumika rasmi mwaka huu.

Vyama hivyo ni Chadema, NCCR – Mageuzi, NLD, UPDP, CCK, ACT – Wazalendo, Chaumma na DP.

Akizungumza kwa niaba ya vyama hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema kesi hiyo namba 3 ya mwaka 2019 imefunguliwa dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na tayari maombi yao yamepokelewa katika mahakama hiyo.

“Tumelazimika kutafuta haki katika Mahakama ya Afrika Mashariki kwa sababu sheria hii inafanya shughuli za kisiasa nchini kuwa jinai kutokana na kila kifungu cha sheria kuweka adhabu ya faini, kifungo au vyote kwa pamoja.

“Tunaiomba mahakama itamke kwamba vifungu tunavyovilalamikia havina hadhi ya kisheria,” alisema Mbowe.

Alisema sheria hiyo inakiuka misingi ya uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa ibara ya 6, 7 na 8 ya mkataba wa uanzishwaji wa jumuiya hiyo.

Mbowe alisema mbali ya kukiukwa kwa Mkataba wa EAC, vifungu vya sheria hiyo vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na misingi ya utawala bora pamoja na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imesaini.

Alivitaja vifungu 11 alivyodai kuwa havina hadhi ya kisheria kuwa ni kifungu cha 3 (b), 3 (g), 5 (A) (i), 5 (B) (i), 6 B (d), 8 (C) (2), 8 D (2), 8 (E), 11 A (2), 23 (7) na 21 (E).  

“Kifungu cha 3 (d) kimempa Msajili wa Vyama vya Siasa jukumu la kusimamia chaguzi za ndani ya vyama ikiwa ni pamoja na teuzi za wagombea wa nafasi mbalimbali.

“Hii inampa msajili mamlaka ya kuingilia vyama na kuviamulia ni nani awe kiongozi wa chama husika au mgombea wa nafasi ya kiserikali kama mgombea urais na ubunge,” alisema Mbowe.

Mbali ya kwenda Mahakama ya Afrika Mashariki vyama hivyo vilisema vinatarajia pia kufungua kesi katika Mahakama Kuu na iwapo vitashindwa vitaendelea hadi Mahakama ya Afrika.

CAG na Ndugai

Katika hatua nyingine, sakata la Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Profesa Mussa Assad na Spika wa Bunge, Job Ndugai, limechukua sura mpya baada ya vyama vinane vya upinzani kumtaka spika Ndugai ajiuzulu.

Juzi Spika Ndugai alisema kitendo cha Profesa Assad kuendelea kulitumia neno dhaifu ni dharau na kejeli kwa mhimili huo muhimu na kumtaka ajiuzulu kwani anampa wakati mgumu Rais John Magufuli.

Akizungumza jana kwa niaba ya vyama hivyo, Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa, alisema taifa limeingizwa kwenye misukosuko bila sababu kwa utashi wa spika.

“Hatua ya kumkataa CAG ni jambo ambalo utekelezaji wake una utata, Bunge linapaswa lisikilize maoni na kuzingatia hoja za wananchi.

“Hatua ya Spika kutangaza kwamba CAG akamuombe radhi Rais anataka kumchanganya Rais katika mgogoro wake, atuambie anataka Rais afanye nini. Baada ya kuona ushauri wake hausikilizwi yeye angeshuka si kung’ang’ania na kugonganisha taasisi…ajiuzulu,” alisema Dovutwa.

Dovutwa pia aliwataka viongozi wakubali kukosolewa na kutokuwa wakali na kusisitiza kuwa wao wanamuunga mkono CAG.

“Leo amemkataa CAG, kesho anaweza kuleta hoja kumkataa Jaji Mkuu au Mkuu wa Majeshi. CAG asimamie msimamo wake, wananchi na kambi ya upinzani tuko pamoja naye,” alisema.

Gazeti hili lilifanya juhudi ya kumtafuta Spika kwa njia ya simu, lakini simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikani.

UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA

Vyama hivyo vimemuomba Waziri wa Tamisemi, kuharakisha kutoa mapitio ya kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kuzipitia na kuona maeneo yanayopaswa kufanyiwa marekebisho.

“Waziri afanye haraka alete mapitio ya kanuni tuyajadili na kuona ni maeneo gani yanapaswa kufanyiwa marekebisho. Tusije tukaletewa hizo kanuni zikiwa zimebaki wiki mbili au tatu,” alisema Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muhabi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles