26.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 16, 2024

Contact us: [email protected]

Sheria mpya ya uwekezaji mbioni kutungwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali imesema ipo mbioni kupeleka bungeni muswada utakaowezesha kutungwa sheria mpya ya uwekezaji itakayokwenda na wakati.

Akizungumza wakati wa kongamano la uwekezaji, Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Profesa Godius Kahyarara, amesema wanafanya maboresho mbalimbali ya kisera na sheria na kwamba sheria ya sasa ilitungwa mwaka 1997 wakati sera ilitungwa mwaka 1996.

Baadhi ya washiriki wa kongamano la uwekezaji lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade).

Kongamano hilo lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo na Biashara Tanzania (TANTRADE) limehusisha baadhi ya washiriki wa maonesho ya 46 ya Sabasaba wakiwemo wanunuzi na wauzaji kutoka ndani na nje.

“Mchakato wa Serikali ulishakamilika, tumeshapitia sheria yote, tumeongea na wadau, tumeangalia vitu gani vipya vya kuingiza katika sheria mpya ya uwekezaji na kwa sasa uko katika taratibu za kupelekwa bungeni,” amesema Profesa Kahyarara.

Amesema mageuzi mengi yamefanyika wakati sheria hiyo imeshatungwa ikiwemo Dira ya Taifa ya 2025 ndiyo maana wameamua kuifanyia maboresho kuiwezesha kwenda na wakati.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji
Tanzania (TIC), Revocatus Rashel, amesema wameanzisha mfumo wa pamoja wa utoaji vibali na leseni kurahisisha shughuli za uwekezaji.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji wa mitaji kutoka nje na kwa mwaka jana ulifikia Dola za Marekani bilioni 1.01 ambalo ni ongezeko la asilimia tatu kutoka mwaka juzi.

“Tanzania ni eneo sahihi la kufanya biashara na uwekezaji, inashika nafasi ya kumi kwa kuwa na maeneo sahihi ya kufanyia biashara na hii yote inatokana na msukumo mzuri wa uongozi wa Rais Samia,” amesema Rashel.

Kwa upande wake Meneja Biashara wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Herieth Nyalusi, amesema kuna viwanja 59 ambavyo vina fursa mbalimbali za uwekezaji.

Amesema pia wana mpango wa kujenga hoteli ya nyota nne katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) pamoja na kuboresha jengo la pili la abiria litakalohudumia abiria milioni 3.5 kutoka milioni 1.5 wa sasa.

Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE, Latifa Khamis, amesema wanatarajia baada ya kongamano hilo kutakuwa na makubaliano yatakayofanyika kupitia sekta za miundombinu, madini na ujenzi.

“Wafanyabiashara wa nje wengi wameshiriki maonesho ya 46, tulisema tusiwaache wakaondoka tuwaongezee fursa, ndiyo maana tuliandaa kongamano hili kuhakikisha fursa walizokuja nazo zinabaki hapa hapa Tanzania,” amesema Latifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles