24.8 C
Dar es Salaam
Friday, October 4, 2024

Contact us: [email protected]

Sheria matumizi bora zana za Kilimo ilete tija kwa wakulima

NA ASHA BANI

HIVI karibuni wadau wa kilimo pamoja na Serikali walianza kupitia rasimu ya kwanza ya sheria ya matumizi bora ya zana za kilimo, ikiwa na lengo la kuwabana waingizaji wa bidhaa bandia.

Katika rasimu hiyo kulikuwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa ikiwa ni pamoja na kubainisha umuhimu wa kuanzisha sheria ya matumizi bora ya zana za kilimo kwa kuangalia upungufu uliopo kwa sasa katika taasisi zinazosimamia ubora wa zana hizo nchini.

Pia rasimu hiyo inaeleza faida zinazopatikana kutokana na sheria hiyo ambapo Shirika la Viwango la Taifa (TBS), linasimamia viwango vya zana za kilimo lakini linashindwa kuangalia utendaji wa zana hizo.

Katika kuangalia hilo, wizara ilipitia sheria za matumizi bora ya zana za kilimo za baadhi ya nchi na kuangalia mafanikio waliyoyapata kwa kuanzisha sheria za matumizi bora ya zana za kilimo hapa nchini.

Imeelezwa na wizara kwamba kwa takwimu za mwaka 2013, zinaonyesha matumizi ya zana za kilimo nchini katika ukatuaji ardhi ilikuwa asilimia 62 kwa mkono, asilimia 24 jembe la wanyama kazi na asilimia 14 ilikuwa ni matrekta.

Hivyo, idadi ya trekta kwa mwaka 2017 ilikuwa 15,554 kwa makubwa na 8, 221 kwa trekta ndogo na kufanya ongezeko la uagizaji wa zana hizo kusababisha kuanzisha sheria ya zana za kilimo itakayolenga kuwasaidia wakulima wake.

Kama ambavyo sera hiyo inaonyesha matumizi bora ya zana za kilimo ni muhimu katika kuongeza na kuendeleza uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini, licha ya kwamba matumizi ya zana bora yameonekana kuwa madogo kutokana na sababu mbalimbali.

Sababu zilizoainishwa na Wizara ya Kilimo ni pamoja na changamoto ya usimamizi bora wa mashine za zana za kilimo, idadi ndogo ya waendesha mitambo waliopata mafunzo na wenye ujuzi, pia teknolojia ya zana za kilimo kushindwa kuendana na mazingira ya nchi.

Hata hivyo, taarifa ya Wizara ya Kilimo imeeleza kuwa kwa mwaka 1930 matrekta mengi yaliingizwa nchini kwa ajili ya kutayarisha na kulima mashamba. Mwaka 1950 kulikuwa na matrekta 2,057 yaliyokuwa yanatumika nchini na yaliyoongezeka hadi kufikia 2,580 kwa mwaka 1960.

Katika mkutano huo wa wadau, Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Mhandisi Methew Mtigumwe, alisema lengo la kufanya hivyo ni kuwapunguzia usumbufu wakulima ambao wamekuwa wakiuziwa zana ambazo hazikidhi ubora.

Anasema hivi sasa nchi ipo katika uchumi wa viwanda hivyo lazima kuwepo na udhibiti utakaoleta tija kwa wakulima na kuwafanya wapate faida badala ya hasara zinazotokana na zana hizo kuharibika kwa kipindi kifupi pindi anapokinunua.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi wa zana za kilimo na umwagiliaji, Joseph Lubiloh, anasema ili nchi iwe na viwanda, uzalishaji unapitia katika sekta ya kilimo hivyo ni vyema zana zikawa bora na endelevu katika kumsaidia mkulima.

Alisema sheria hiyo itasaidia kuwabana wauzaji, wasambazaji na kuwasaidia watumiaji kwa kuwa watakuwa na uhakika wa uzalishaji pia.

Alisema kwa sasa Serikali inatoa mazingira wezeshi kwa kupitia vyama vyao kuwakopesha wakulima pembejeo zitakazowakwamua kiuchumi.

Naye Meneja wa Kampuni ya MeTL Agriculture, Yahya Sagati, alisema sheria hiyo ikisimamiwa na kutekelezwa vizuri itawasaidia wakulima hata kudhibiti wauzaji wa zana feki.

Kutokana na matumizi bora ya zana za kilimo, naamini uchumi wetu utaboreshwa, uzalishaji wa mazao yataongezeka na kuwanufaisha wakulima kwa kuongeza kipato kutokana na mazao mengi na kuyaongezea thamani kwa usindikaji.

Uzalishaji wa malighafi za viwanda utaongezeka na kuwavutia wawekezaji kujenga viwanda vya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa za viwandani. Ili kukidhi matarajio hayo ya kuleta mapinduzi ya dhati katika kilimo, matumizi bora ya zana yanahitajika na hivyo uwepo wa sheria na mwongozo wa biashara na matumizi ya zana za kilimo ni muhimu zaidi katika kipindi hiki kuliko wakati mwingine wowote uliopita

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles