25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

SHEIN: Z’BAR TUKIKATIWA UMEME TUTATUMIA VIBATARI

Na WAANDISHI WETU – ZANZIBAR/DAR ES SALAAM


RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema iwapo Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) litaikatia umeme Zanzibar kutokana na deni wanalodaiwa, wataweza kurudi katika matumizi ya asili ambayo ni kutumia vibatari kupata mwanga.

Dk. Shein aliyasema hayo mara baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Amaan Abeid Karume, akitokea nchini Indonesia katika mkutano maalumu aliomuwakilisha Rais Dk. John Magufuli.

Kauli hiyo imekuja wakati Tanesco jana ikiwa imetoa siku 14 kwa wadaiwa wote sugu, ikiwa ni pamoja na Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), linalodaiwa Sh bilioni 127, kulipa deni hilo ndani ya muda huo kabla ya kukatiwa umeme.

Wiki iliyopita, Rais Magufuli aliiagiza Tanesco kukata umeme kwa wadaiwa wote sugu, akisema hata kama Ikulu ya Magogoni inadaiwa, nayo pia ikatiwe nishati hiyo.

Jana mara baada ya Dk. Shein kuwasili, alizungumzia mafanikio ya safari yake ikiwa ni pamoja na mipango ya viwanda, kauli iliyofanya waandishi kuuliza viwanda hivyo vitaendeshwa vipi ilihali Tanesco imetangaza kuikatia umeme Zanzibar.

Kutokana na swali hilo alisema: “Naamini Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Serikali ya kiungwana, inayojali watu wake, hivyo haiwezi kufanya hivyo kwenye suala hili la kuzima umeme visiwani Zanzibar na iwapo ikitokea umezimwa, Zanzibar watakuwa tayari kurudi kwenye matumizi ya vibatari.”

Alisema akiwa safarini alisoma magazeti mawili yaliyoandika juu ya Zanzibar kukatiwa umeme, lakini haamini kama taarifa hizo zina ukweli, huenda waandishi walinukuu vibaya vyanzo vya taarifa hiyo.

“Siamini kama umeme wanaweza kuzima, lakini natungojee wazime tuone,” alisema Dk. Shein.

Alisema atashangazwa iwapo umeme utakatwa, ikizingatiwa mahusiano mazuri yaliyopo baina ya pande mbili hizi zinazounda Tanzania.

Alieleza kwa kipindi cha miaka mingi, ikiwa ni pamoja na wakati yeye akiwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Zanzibar imekuwa ikidaiwa na Tanesco na wamekuwa wakilipa kwa utaratibu maalumu.

Alisema suala la kudaiwa si geni na lipo kwa muda mrefu na wao kama Serikali hawajawahi kukataa kulipa, hivyo ni utaratibu maalumu ambao unapaswa kutumika ili kuondoa hali hiyo.

 

SIKU 14

Wadaiwa sugu wa Tanesco, wakiwamo Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), wizara na taasisi za Serikali, wamepewa siku 14 kulipa madeni yao kabla kukatiwa huduma.

Hayo yalisemwa na Kaimu Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Dar es Salaam jana.

Katika mkutano huo uliohusisha vyombo vichache vya habari – televisheni moja binafsi, moja ya Serikali, magazeti ya Serikali na ya kampuni moja binafsi, Dk. Mwinuka alisema hadi sasa shirika hilo linadai zaidi ya Sh bilioni 275 kwa Zeco, Wizara, Taasisi za Serikali na makampuni ya watu binafsi.

Dk. Mwinuka alisema jambo hilo limechangia kurudisha nyuma utendaji wa shirika hilo katika kusambaza huduma ya umeme nchini.

Alisema kutokana na hali hiyo, baada ya muda waliotoa kwisha bila deni hilo kulipwa, Tanesco itachukua uamuzi mgumu wa kuwakatia umeme wadaiwa hao.

Katika deni hilo, Zeco inadaiwa Sh bilioni 127, mashirika ya serikali, wizara na taasisi  Sh bilioni  52, huku kampuni binafsi na wateja wadogo wakidaiwa Sh bilioni 94.

“Tumetoa siku 14 kwa wadaiwa sugu wote wa Tanesco, wakiwamo Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco) ambao tunawadai Sh bilioni 127 hadi Januari mwaka huu, wizara na taasisi za Serikali ambazo na zenyewe tunazidai, wanapaswa kulipa deni lao ili kuepusha usumbufu wa kukatiwa umeme,” alisema Dk. Mwinuka.

Alisema hadi sasa wameshatoa notisi ya siku 14 kwa wadaiwa hao ili waweze kulipa madeni yao na watakaoshindwa kufanya hivyo, watakuwa wamekaidi notisi hiyo.

Dk. Mwinuka alisema malimbikizo ya madeni hayo yamekuwa yakikwamisha jitihada za utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya msingi ndani ya shirika hilo.

Alisema shirika hilo linahitaji fedha kwa uendeshaji wa shughuli mbalimbali, ikiwamo matengenezo ya miundombinu na utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Dk. Mwinuka alisema mkakati wao ni kuhakikisha wanakusanya madeni hayo na fedha zitakazopatikana zisaidie kufanya shughuli za usambazaji umeme ili huduma hiyo iwafikie watu wengi zaidi.

Alisema upatikanaji wa umeme utasaidia kuchochea maendeleo na kusaidia ukuaji wa sekta mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme.

 

Taarifa hii imeandaliwa na MUHAMMED KHAMIS (UOI – ZANZIBAR) na PATRICIA KIMELEMETA (DAR ES SALAAM)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles