20.5 C
Dar es Salaam
Saturday, August 20, 2022

Shein: CCM kuendelea kuhubiri umoja

Na Mwandishi Wetu- Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema juhudi za Serikali za kuwahamasisha, kushirikiana na wananchi  na asasi mbali mbali kwa lengo la  kudumisha amani, ni utekelezaji wa miongozo ya Ilani ya CCM ya uchaguzi ya mwaka 2015/20  na ile ya 2020/25.

Rais Dk. Shein, alisema  hayo wakati wa uzinduzi wa kongamano la amani kitaifa lililofanyika  mjini Unguja jana.

Alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitaendelea kuhubiri umoja na mshikamano na kupinga ubaguzi wa aina zote na kuliweka suala la kulinda na kudumisha amani kuwa kipaumbele chake katika Ilani zilizopita na zitakazokuja.

Alinukuu kifungu cha  Ilani ya 2015/20  (Ibara ya 127), kinachobainiusha dhamira ya  kuendeleza sera ya kuwaunganisha wananchi wa Zanzibar katika kipindi cha 2015/20, CCM pamoja na kuendelea kuwa muumin wa kweli wa amani na utulivu ili kuimarisha mafanikio yaliokwisha kupatikana.

Alisema chama kimeielekeza Serikali kuendeleza jitihada za kuihamasisha jamii juu ya umuhimu wa amani, umoja na mshikamano ili kujenga mazingira ya kuaminiana, kuvumiliana na kushirikiana katika masuala mbali mbali ya kijamii.

Alisema kimeielekeza Serikali kuendelea kupiga vita na kudhibiti vitendo vya ubaguzi vinavyojitokeza katika sehemu za utoaji huduma za kiuchumi, kisiasa na kijamii miongoni mwa wananchi.

 Alisema kongamano hilo, ni muhimu kwa wananchi wa Zanzibar kwa kuzingatia kuwa maudhui yake makuu yanahusu wajibu wa Serikali wa kulinda amani na usalama kama ilivyoelezwa ndani ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.

Alisema kazi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ni kutunza amani iliopo pamoja na kuwashughulikia wale wote watakaovuruga amani hiyo.

Alisema katika kipindi cha uchaguzi, nchi nyingi duniani hukumbwa na majaribio yenye kuashiria uvunjifu wa amani, ambapo baadhi yake hushindwa kudhibiti matokeo hayo  na kupata athari mbali mbali, ikiwemo za kiuchumi.

Alisema athari nyingine zinazopatikana kutokana na uvunjifu wa amani ni kwa baadhi ya vyama vya siasa kufanya kampeni zenye kuwagawa watu kwa misingi ya dini zao, makabila, uwezo au sehemu wanazotoka.

Aliwakumbusha wananchi umuhimu wa kutafakari na kuepuka makosa  ya kuwachagua viongozi wasio na dhamira ya kuendeleza umoja na mshikamano wa Wazanzibari.

Aliwataka kuepuka kuwachagua viongozi wasio na uwezo au uzoefu katika kulinda na kudumisha amani, kwani lengo lao ni kuwagawa.

Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd aliwataka Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla kuienzi amani iliopo, kwa kutambua kuwa kuna watu wengi wanaolionea wivu Taifa hili kutokana na tunu hiyo adhimu.

Mgombea urasi wa CCM, Dk. Hussein   Mwinyi katika salamu zake, alisema wakati huu vyama vya siasa vikinadi sera zao kuelekea uchaguzi mkuu baadae mwezi huu, ni vyema kusisitiza uwepo amani nchini, kwa kigezo kuwa hakuna maendeleo yoyote yatakayoweza kupatikana bila amani.

“Amani huletwa na utulivu wa wananchi wake na sio kundi kubwa la askari au vifaa vya kivita”, alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
199,058FollowersFollow
551,000SubscribersSubscribe

Latest Articles