23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Sheikh Ponda azindua kitabu cha Maisha na Changamoto

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Watanzania wamehimizwa kubadilika kwa kutumia muda mwingi katika kusoma na kuandika vitabu badala ya kujikita katika kusikiliza michezo muda wote.

Sheikh Ponda Issa Ponda.

Hayo yamebainishwa Dar es Salaam Septemba 3, 2022 na Katibu wa Shura ya Maimamu nchini Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu chake cha Maisha na Changamoto hafla ambayo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.

Amesema amefikia hatua ya kuandika kitabu hicho kwa ajili ya kuelimisha jamii na kulinda yale yaliyofanyika.

“Nililipa kipaumbele suala la uandishi wa kitabu sababu nilifikiria zaidi ya kuelimisha na inafanya yale tuliyoyafanya yadumu ndiyo sababu hadi leo tunasoma maandiko ya watu wengine ambayo yameandikwa muda mrefu.

“Pia kuandika kuwasaidia kutatua changamoto mbalimbali, leo Tanzania unaweza kusikiliza vipindi vya michezo kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa 12 jioni, hivyo tunapaswa kubadilika na kutumia vyombo vya habari kutoa elimu,” amesema Sheikh Ponda na kuongeza kuwa kumekuwa na changamoto kwenye jamii kutokana na mazingira yanayoizunguka.

Amesema mwaka 2012 alianza kuandika kitabu hicho hadi ilipofikia mwaka 2021 akawa amefikisha kitabu 15 vyenye sura na mada tofautitofauti.

“Ndani ya kipindi hicho kumetokea mambo mengi ikiwamo kukamatwa na mambo mengine ila ilipofika 2021 nikawa nimekamilisha hiki kimoja ambacho tunakizindua leo, pia kuna kitabu cha Pitio la Zanzibar ambacho kimefikia asilimia 90 sawa na kile cha Matukio na Habari ambacho pia kimefikia asilimilia 90 pia kuna vitabu kama Ukweli katika Utafiti, Mahakama ya Kazi.

“Pia kuna vitabu kama Mkono wa Dola na “Kiswahili chaweka Rehani” suala la lugha ya Kiswahili ambapo kwa bahati mbaya hapa kwetu Tanzania lugha hii imeshindwa kutumiwa na haitendewi haki kwani imefanywa kukosa uenyeji wake,” amesema Shaikh Ponda.

Akizungumzia kitabu cha Waliopotea Tanzania amesema kuwa kina lengo la kuisaidia Serikali kuhusu hali ilivyo na nikwa namna gani inaweza kukabiliana na changamoto hiyo.

“Lengo la mkutano wa leo ni kwamba tunahamasisha viongozi kuandika vitabu, lakini niseme tu kwamba wakati flani kulikuwa na mpango kwa serikali kuanzisha maktaba mtandao lakini baadae ikaonekana kwamba gharama zake ni kubwa.

“Lakini niwaeleze tu kwamba binafsi nilikaa na wataalamu tukaingia makubaliano ya mkataba kwa ajili ya kutengeneza maktaba hiyo mtandao itakayofahamika kama Ponda Issa Ponda Library habari njema nikwamba itazinduliwa Oktoba, mwaka huu itakayoenda sambamba na uzinduzi wa programu tumishi,” amesema Sheikh Ponda.

Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Azaveli Lwaitama, alisema kuwa kuandika kitabu ni kitu kizuri lakini vitabu vya wale waliopitia misukosuko kama Sheikh Ponda lazima kutakuwa na jambo la kujifunza, hivyo hii inamaana kwamba anahimiza hata hata ambao wamepitia changamoto hata za kimaisha nje ya siasa kuandika vitabu,” amesema Dk. Lwaitama.

Upande wake Mwandishi mstaafu, Generali Ulimwengu alisema kuwa Waafrika wamekuwa hawana utamaduni wa kusoma vitabu kwani imekuwa ikitazama vitabu kama Mama mkwe.

“Unajua mkwe wako huwezi kumfunua hivyo hata kwenye usomaji imekuwa hivyohivyo jambo ambalo tunapaswa kulikataa.

“Na hii siyo Tanzania tu bali Afrika Mashariki kwa ujumla, pia hata Nigeria imekuwa changamoto kwani hata elimu wanayoipata bado haiwasaidii hatua ambayo imechochea migogoro,” amesema Ulimwengu na kuongeza kuwa:

“Sababu ambayo inasabisha tusisome vitabu wengi wanasema ni hali ngumu ya maisha jambo ambalo siyo kweli kwani Sh 20,000 ya kununua kitabu ni sawa na milo mitatu tu ya wali na kuku. Hivyo, tunavisingizio vingi, lakini ukweli ni kwamba tunatumia hela nyingi sana katika starehe kuliko vitu vya msingi, na inashangaza kuona tunafurahia ilihali maisha yamekuwa magumu,” amesema Ulimwengu.

Upande wake Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema ni wazi kuna changamoto kwa Bara la Afrika kusoma vitabu nakwamba kama Taifa inapaswa kuongozwa na kitabu kimoja ambacho ni Katiba.

“Tuanze kuandika iwe kwa makala, au mamna yoyote ile juu ya Tanzania  tunatoitaka kupitia katiba mpya,” amesema Mnyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles