27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

SHEIKH AWATETEA WAISLAMU WALIOPO MAGEREZANI

Na Mwandishi Wetu


VYOMBO vya dola vimetakiwa kuharakisha upelelezi wa kesi za waislamu wakiwamo masheikh na maimamu waliopo magerezani, ili haki iweze kutendeka.

Wito huo ulitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kiislamu ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatima ya waislamu na baadhi ya masheikh waliopo rumande kwa tuhuma za ugaidi, ambao wanaendelea kuteseka.

Alisema umefika wakati kesi hizo ziharakishwe ili wakosaji watiwe hatiani na wasiokuwa na makosa waachiliwe huru, kwani waislamu zaidi ya 200 wanashikiliwa katika magereza mbalimbali nchini kwa makosa ya kubambikiwa.

Sheikh huyo alisema, waislamu hao wanasota magerezani na wengine makosa yao yakiwa hayajulikani, jambo ambalo ni kinyume na haki za binadamu na Katiba ya nchi.

Kiongozi huyo aliwataka waislamu kote nchini kuungana kupigania haki za masheikh na waislamu waliopo magerezani.

“Tunawaomba Waislamu kuendelea kuwachangia Waislamu wenzetu walioko magerezani wakitumikia vifungo visivyokuwa rasmi pamoja na kuwatembelea mpaka pale watakapotiwa hatiani na mahakama.

“Hivi kweli sisi ni waislamu wa hakika wakati waislamu wenzetu masheikh zetu wanateseka na kushikiliwa bila  ukomo na hawasikilizwi kwa lolote na wakati huo huo sisi tumebwetweka na wala hatushughulishwi na madhila yanayowakuta kisha tunasema kuwa Waislamu wote ni ndugu?,” alihoji.

Pamoja na hayo Sheikh Khalifa alitoa wito kwa Serikali. “Tunaitaka Serikali pamoja na vyombo vyote vinavyohusika na utungaji wa sheria wairejee upya sheria ya ugaidi ya mwaka 2002 ili kuondoa mapungufu ambayo kwa mujibu wa Katiba yetu yanaweza kumaanisha ubaguzi miongoni mwa raia hususan Waislamu ambao ndio waathirika pekee wa sheria hiyo,” alisema.

Sheikh Khalifa alisema taasisi yake inaunga mkono kauli ya Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa aliyoitoa mwezi uliopita, ambapo alimtaka Rais Dk. John Magufuli, kutafakari juu ya hatima ya masheikh wa Jumuiya ya Uamsho wanaosota gerezani kwa zaidi ya miaka mine sasa bila kesi yao kusikilizwa.

“Kama Lowassa aliyasema yale kisiasa sisi huko hatupo ispokua tunaunga mkono alichosema kwa kua kinalenga kutetea haki za watu.

“Katika hili tunamwomba Rais Magufuli alitazame kwa jicho la tatu, akina Sheikh Farid alikamatwa tangu mwaka 2012 mauaji ya Kibiti yameibuka 2017 hawa watu wanahusikaje?

“Tunajua Rais ndiye mkuu wa nchi taarifa nyingi anazo, lakini taarifa nyingine anazopewa si sahihi. Hawa masheikh walikamatwa Zanzibar na sababu za kukamatwa kwao zilitolewa na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tofauti na hizi anazosema Rais Magufuli.

“Kimsingi sisi hatusemi waachiliwe tu, bali tunataka mashitaka yao yasomwe mahakamani, makosa yao yajulijkane na wao wapate fursa ya kujitetea kama ni kuhukumiwa wahukumiwe au waachiwe huru kuliko kuendelea kuwatesa.

“Hatukumchagua Rais Magufuli kuwa mfalme, bali tulimchagua kuwa mtumishi. Kuwa mtumishi ni pamoja na kujali na kuthamani haki za watu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles