23.8 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Shehena ya viungo vya binadamu yanaswa

mabaki ya miili ya watu
Wananchi wakiangalia mifuko yenye viungo mbalimbali vya binadamu vilivyokutwa katika Bonde la Mweni Mpiji wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam jana. Picha ndogo kushoto ni polisi wakipakia viungo hivyo. Picha zote na Deus Mhagale

Na Fredy Azzah, Dar es Salaam

NI mshtuko , binadamu tumefikia hapa? Ndiyo maneno yaliyowatoka mamia ya wananchi waliofika katika eneo la Bonde la Mbweni Mpiji Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, baada ya  kushuhudia shehena ya mifuko iliyokuwa na viungo vya binadamu.

Katika eneo hilo, MTANZANIA ilishuhudia mifuko mikubwa  mieusi  ya nailoni  ikiwa na viungo mbalimbali vya binadamu vikiwa vimechunwa ngozi.

Viungo hivyo ambavyo vilionekana  nyama zake zikiwa zimekauka ni pamoja na mafuvu ya vichwa, sehemu ya kifua cha binadamu, miguu, mikono, moyo na  mapafu.

Licha ya baadhi ya viungo kuonekana wazi kwa juu, vilikuwa havitoi  harufu  jambo lililotafsiriwa kuwa vilikuwa vimepuliziwa dawa  kali ya kuondoa harufu.

Baadhi ya mashududa wa tukio hilo, waliiambia MTANZANIA kuwa miili hiyo ilitupwa  eneo hilo  tangu Jumapili Julai 20, mwaka huu.

Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Super Kaijunga (45) alisema  alikuwa mtu wa kwanza kuona viungo hivyo.

Alisema hali hiyo, ilisababisha  kuwaita wananchi wengine wanaoishi jirani na eneo hilo kabla ya kutoa taarifa kwa jeshi la polisi.

Alisema shehena hiyo, ilitupwa  eneo hilo usiku wa kuamkia Jumapili kwa sababu, ingawa wananchi wengi wanapita eneo hilo hawakutambua ni kitu gani.

Kutokana na shehena hiyo kutotoa harufu, hakuna mtu  aliyejishughulisha kuigusa mifuko hiyo  mpaka jana jioni, baada ya baadhi ya wanawake wanaogonga kokoto katika eneo hilo walipokwenda  eneo hilo.

Alisema wanawake hao, walipofike eneo hilo walianza kufungua mifuko hiyo kwa lengo la kuichukua kwa ajili ya kuhifadhia kokoto ndipo walipokutana na viungo vya binadamu.

“Mimi jana (juzi)  mpaka nimelala hapa na hii mifuko ilikuwa hapa hakuna aliyeigusa. Jana ndiyo dada mmoja akaniita akaniambia nije anionyeshe kitu cha ajabu. Ndiyo tukaja hapa tukaona hivi viungo nikaanza kutoa taarifa,” alisema Kajuna.

Kutokana na kusambaa kwa taarifa za tukio hilo, wananchi wengi walifahamu jana kuanzia saa 11 jioni hali iliyowalazimu kutoa taarifa  katika kituo cha  Bunju na Wazo.

Polisi  walifika  eneo la tukio na kuanza kazi  ya kuchukua mabaki ya miili na kuijaza kwenye mifuko kisha  kuipeleka katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.

Pamoja na vitu vingine, mifuko hiyo mikubwa  ndani  ilikuwa na vitaambaa maalumu ambavyo huvaliwa kifuani na madaktari kwa ajili ya kuzuia uchafu pindi wanapofanya upasuaji wa mgonjwa.

Kutokana na tukio hilo, wananchi wengi  wamejiuliza maswali mengi huku baadhi wakisema kuwa viungo hivyo yawezekana  vilitoka katika moja ya hospitali kubwa.

“Kama viungo hivi ni vya hospitali kwa nini vitupwe huku wakati huwa kuna sehemu za kuteketeza vitu kama hivi na kwa nini vichunwe ngozi,” walisema baadhi ya wananchi waliokuwa katika eneo hilo

Akizungumza na MTANZANIA kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni  Camilius Wambura  alisema mifuko hiyo yenye viungo vya binadamu  iliyokutwa  eneo  la tukio ni zaidi ya 85.

Alisema  baadhi ya viungo vilivyokutwa ni pamoja   miguu,  mikono na vichwa.

Alisema Jeshi la Polisi linalazimika kuvipeleka viungo hivyo Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.

Baadhi ya wananchi walisema vungo hivyo vilifikishwa hapo na gari dogo maarufu kama kirikuu.

Kutokana na hali hiyo, gari moja la aina hiyo lilikuwa likienda kwenye eneo hilo na lilipoona watu liligeuza na kukimbia kabla ya kuzuiwa na vijana waendesha pikipiki.

Baada ya kukamatwa lilifikishwa katika kituo cha polisi Bunju hali iliyofanya wananchi kujaa wakisema  gari hilo lilikuwa limebeba viungo vingine.

Hata hivyo baada ya polisi kulikagua gari hilo walibaini lilikuwa limebeba mayai mabovu na vifaraka waliokufa walivyokuwa wakienda kuvitupa katika eneo lililokuwa imetupwa viungo hivyo.

Kutokana na taharuki hiyo,polisi walilazimika kufyatua risasi za moto hewani ili kutawanya umati wa wananchi waliokuwa wamefurika kwenye eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

2 COMMENTS

    • Maoni yangu nikwamba serikali yetu imeweza kuingia aibu sana! katka jambo kama hili ambalo kwa tanzania nijambo lakutia aibu. Sasa mimi naishauri serikali husisani wizara ya afya ichukue hatua kali sana zakisheria kwa wote walio shiriki katka aibu hii.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,718FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles