Na Fredy Azzah, Dar es Salaam
NI mshtuko , binadamu tumefikia hapa? Ndiyo maneno yaliyowatoka mamia ya wananchi waliofika katika eneo la Bonde la Mbweni Mpiji Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, baada ya kushuhudia shehena ya mifuko iliyokuwa na viungo vya binadamu.
Katika eneo hilo, MTANZANIA ilishuhudia mifuko mikubwa mieusi ya nailoni ikiwa na viungo mbalimbali vya binadamu vikiwa vimechunwa ngozi.
Viungo hivyo ambavyo vilionekana nyama zake zikiwa zimekauka ni pamoja na mafuvu ya vichwa, sehemu ya kifua cha binadamu, miguu, mikono, moyo na mapafu.
Licha ya baadhi ya viungo kuonekana wazi kwa juu, vilikuwa havitoi harufu jambo lililotafsiriwa kuwa vilikuwa vimepuliziwa dawa kali ya kuondoa harufu.
Baadhi ya mashududa wa tukio hilo, waliiambia MTANZANIA kuwa miili hiyo ilitupwa eneo hilo tangu Jumapili Julai 20, mwaka huu.
Mmoja wa shuhuda wa tukio hilo, Super Kaijunga (45) alisema alikuwa mtu wa kwanza kuona viungo hivyo.
Alisema hali hiyo, ilisababisha kuwaita wananchi wengine wanaoishi jirani na eneo hilo kabla ya kutoa taarifa kwa jeshi la polisi.
Alisema shehena hiyo, ilitupwa eneo hilo usiku wa kuamkia Jumapili kwa sababu, ingawa wananchi wengi wanapita eneo hilo hawakutambua ni kitu gani.
Kutokana na shehena hiyo kutotoa harufu, hakuna mtu aliyejishughulisha kuigusa mifuko hiyo mpaka jana jioni, baada ya baadhi ya wanawake wanaogonga kokoto katika eneo hilo walipokwenda eneo hilo.
Alisema wanawake hao, walipofike eneo hilo walianza kufungua mifuko hiyo kwa lengo la kuichukua kwa ajili ya kuhifadhia kokoto ndipo walipokutana na viungo vya binadamu.
“Mimi jana (juzi) mpaka nimelala hapa na hii mifuko ilikuwa hapa hakuna aliyeigusa. Jana ndiyo dada mmoja akaniita akaniambia nije anionyeshe kitu cha ajabu. Ndiyo tukaja hapa tukaona hivi viungo nikaanza kutoa taarifa,” alisema Kajuna.
Kutokana na kusambaa kwa taarifa za tukio hilo, wananchi wengi walifahamu jana kuanzia saa 11 jioni hali iliyowalazimu kutoa taarifa katika kituo cha Bunju na Wazo.
Polisi walifika eneo la tukio na kuanza kazi ya kuchukua mabaki ya miili na kuijaza kwenye mifuko kisha kuipeleka katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
Pamoja na vitu vingine, mifuko hiyo mikubwa ndani ilikuwa na vitaambaa maalumu ambavyo huvaliwa kifuani na madaktari kwa ajili ya kuzuia uchafu pindi wanapofanya upasuaji wa mgonjwa.
Kutokana na tukio hilo, wananchi wengi wamejiuliza maswali mengi huku baadhi wakisema kuwa viungo hivyo yawezekana vilitoka katika moja ya hospitali kubwa.
“Kama viungo hivi ni vya hospitali kwa nini vitupwe huku wakati huwa kuna sehemu za kuteketeza vitu kama hivi na kwa nini vichunwe ngozi,” walisema baadhi ya wananchi waliokuwa katika eneo hilo
Akizungumza na MTANZANIA kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni Camilius Wambura alisema mifuko hiyo yenye viungo vya binadamu iliyokutwa eneo la tukio ni zaidi ya 85.
Alisema baadhi ya viungo vilivyokutwa ni pamoja miguu, mikono na vichwa.
Alisema Jeshi la Polisi linalazimika kuvipeleka viungo hivyo Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi.
Baadhi ya wananchi walisema vungo hivyo vilifikishwa hapo na gari dogo maarufu kama kirikuu.
Kutokana na hali hiyo, gari moja la aina hiyo lilikuwa likienda kwenye eneo hilo na lilipoona watu liligeuza na kukimbia kabla ya kuzuiwa na vijana waendesha pikipiki.
Baada ya kukamatwa lilifikishwa katika kituo cha polisi Bunju hali iliyofanya wananchi kujaa wakisema gari hilo lilikuwa limebeba viungo vingine.
Hata hivyo baada ya polisi kulikagua gari hilo walibaini lilikuwa limebeba mayai mabovu na vifaraka waliokufa walivyokuwa wakienda kuvitupa katika eneo lililokuwa imetupwa viungo hivyo.
Kutokana na taharuki hiyo,polisi walilazimika kufyatua risasi za moto hewani ili kutawanya umati wa wananchi waliokuwa wamefurika kwenye eneo hilo.
Bado utupaji wa viungo hivi vya binadamu unasababisha maswali mengi. Tuwe wavumilivu vyombo vinnavyohusika vifanye uchunguzi wa kina kwanza.
Maoni yangu nikwamba serikali yetu imeweza kuingia aibu sana! katka jambo kama hili ambalo kwa tanzania nijambo lakutia aibu. Sasa mimi naishauri serikali husisani wizara ya afya ichukue hatua kali sana zakisheria kwa wote walio shiriki katka aibu hii.