30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Shanta kuanza uzalishaji wa dhahabu Singida 2023

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

MGODI wa Kati wa uchimbaji wa madini ya Dhahabu wa Shanta wa Singida unatarajiwa kuanza rasmi uzalishaji mwanzoni mwa mwaka 2023 mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya mgodi huo.

Meneja Mkuu wa mradi huo, Mhandisi Jiten Divecha ameyasema hayo Mei 13, 2022 kwa Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa wakati alipotembelea na kukagua Maendeleo ya Mradi wa Mgodi wa Kati wa Dhababu wa Singida (Singida Gold Mine) unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Mining Company Limited uliyopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.

Divecha amesema, kwa sasa mgodi umeendelea kutoa fursa mbalimbali za ajira kwa Watanzania pamoja na kununua bidhaa za Kitanzania.

Akizungumza, mara baada ya kukagua maeneo ya uchimbaji katika mgodi huo, Dk. Kiruswa ameagiza uongozi kuhakikisha wanamaliza changamoto zote zinazokwamisha kuanza kwa mradi huo ili uchimbaji uanze kwa haraka.

Amesema, wananchi wa Ikungi na wakazi wa Singida wanatarajia kuona mgodi huo unaanza kazi ili wananchi waweze kunufaika na uwepo wa mgodi katika jamii yao.

Pia, Dk. Kiruswa ameipongeza Kampuni ya ya Uchimbaji Madini ya Shanta kwa uwekezaji mkubwa wanaoendelea kuufanya katika mgodi huo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya mgodi, ajira zinazotolewa, afya na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Vile vile, Dk. Kiruswa ameuagiza mgodi wa Shanta kuandaa na kutekeleza mpango wa uchangiaji wa kampuni yao kwenye jamii (CSR) kwa mujibu wa Sheria.

Amesema, wanatakiwa kuhakikisha kama wawekezaji jamii inayowazunguka inanufaika na mradi husika huku akifurahishwa na Sheria ya Local Content inavyotekelezwa na mgodi huo.

“Nimefurahishwa na mpango wa Local Content, nimetembea hapa sijaona hata mgeni mmoja, wanaofanya kazi hapa wote ni Watanzania, lakini pia mnatumia rasilimali zinazopatikana hapa hapa, nimesikia hata maharage yanatoka hapa,”amesema Dk. Kiruswa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu amemueleza Dk. Kiruswa kuwa, wananchi wa Singida wanatamani mradi huo uanze mara moja ili waweze kunufaika na mradi huo.

Amesema, mradi utakapoanza utaleta maendeleo kwa jamii inayozunguka pamoja na kuongeza mapato kwa Serikali. 

Wengine waliohudhuria ziara ya Naibu Waziri wa Madini ni viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ikungi, viongozi wa vijiji na kata wanaozunguka eneo la mradi na wadau wa Sekta ya Madini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles