MWANDISHI WETU-MOROGORO
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro kimesema kuwa genge la wapinga Mapinduzi ya Zanzibar ndilo lililopanga njama hadi kumuua Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume na sasa mabaki yake ndiyo yanayoendeleza chuki, uhasama na ukorofi wa kisiasa nchini.
Kwamba wauaji licha ya kuyapoteza maisha ya kiongozi huyo shupavu, lakini pia lengo ilikuwa ni kukwamisha mchakato wa malengo na sera za ASP zisifike azma ya kuleta maendeleo kusudiwa.
Msimamo huo umetolewa jana na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, alipoulizwa na gazeti hili kuhusu mtazamo wake katika miaka 48 ya kumbukizi ya mauaji dhidi ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, ambaye aliuawa Aprili 7, 1972 .
Alisema hadi sasa mabaki ya wapinzani waliokizuia Chama cha ASP kisishike utawala kwa njia za uchaguzi, hata pale yalipofanyika mapinduzi, walichukizwa kuiona Serikali ya wazalendo ikisimamia vyema maendeleo ya kisiasa, kujenga umoja na kukuza uchumi.
Shaka alisema sera makini, uongozi bora, siasa safi na ustawi wa maisha ya watu ulioshamirisha maendeleo ya kisekta chini ya ASP, hayakuwapendezesha wapinzani na kuamua kumuua kiongozi ambaye alikuwa mchapakazi, mwenye busara, dhamira na shabaha ya kuutumikia umma.
“Aprili 7, 1972 Zanzibar ilikutwa na msiba mkubwa wa kumpoteza jemedari wake hayati Mzee Abeid Karume, wapinzani wa ASP wameyakatisha maisha yake baada ya kuona akiongoza na kujenga ustawi wa maendeleo. Mabaki ya watu hao hadi sasa ndiyo wanaoeneza chokochoko, hasama na ukorofi wa kisiasa,” alisema Shaka.
Aidha Shaka alieleza kuwa vizazi vyote kikiwemo kizazi cha sasa na vijavyo, vitaendelea kusoma, kuihifadhi na kuifuatilia historia ya ASP pamoja na harakati zilizoleta ukombozi hadi kufanyika mapinduzi na katu hakitasahau kifo cha shujaa wa huyo.
Alisema ingawa miaka 48 imepita tangu rais huyo kuuawa, Watanzania wema bado wanaukumbuka msiba wa kumpoteza Mzee Karume ambaye maisha yake yalidhulumiwa kikatili na kundi la maadui na vibaraka waliotumiwa na mabeberu.
“Tutaendelea kumkumbuka mzee wetu milele, tunaamini kilichokufa ni kiwiliwili chake, fikra, malengo na shabaha za Serikali ya ASP zitadumishwa toka kizazi kimoja hadi kingine, kazi ya kulinda na kuisimamia misingi ya Mapinduzi itaendelezwa bila woga,” alisema Shaka.
Alikumbusha kuwa wanawatambua kwa asili na majina yao, bibi na babu zao, walivyoshiriki kuipinga ASP tokea mwaka 1957 isifanikiwe kushika utawala kwa njia za uchaguzi hadi wazee walipoona ipo haja ya kuupindua utawala wa kisultani.
Shaka alisisitiza kuwa CCM itamuenzi, kumkumbuka na kumheshimu kiongozi huyo kwa sababu ndiye pekee barani Afrika aliyekuwa tayari kutekeleza dhana ya Muungano, hatimaye kuafiki na kumpisha mwenzake Mwalimu Julius Nyerere awe rais naye abaki kuwa Makamu wa Rais.
Alisema kuwa pamoja na kufanyika mikutano mingi ya Pan Africanism (umajumui), iliyojadili na kutolewa maazimio ya kuunda dola moja Afrika, mara baada ya nchi za kiafrika kupata uhuru, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ndio waliokubali kutekeleza maazimio hayo.