26.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 1, 2021

SHAKA: UVCCM JIKO LA KUPIKA VIONGOZI

Na AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM 


KAIMU Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, amesema jumuiya hiyo ni jiko la kupika vijana wanaotarajiwa kushika madaraka siku za usoni.

 Alisema hakuna kijana anayejiunga na jumuiya hiyo akiwa na ufahamu mkubwa wa kisiasa, hivyo hoja ya kusema kila anayeshika nafasi UVCCM ni bingwa ni dhaifu.

Akitambulisha wajumbe watano wa sekretarieti  walioteuliwa na Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya hiyo Taifa, Dar es Salaam jana, Shaka alisema kamati hiyo iliyokutana Aprili 18, mwaka huu ndiyo iliyofanya uteuzi wa wajumbe hao.

Miongoni mwa wajumbe hao ni aliyekuwa Miss Tanzania namba mbili 2006, Jokate Mwegelo kuwa Kaimu Katibu wa Idara ya Uhamasishaji Chipukizi Taifa.

 “Jumuiya hii ni tanuru, benki na jiko linalowapiga msasa vijana, ili kuwa warithi wa madaraka ya kiserikali  na kisiasa.

“Kuanzia ngazi ya tawi, kata, jimbo, wilaya, mkoa hadi Taifa, hakuna kijana anayejiunga akiwa na ujuzi uliokamilika ama kuwa na ufahamu wa kila jambo, wote hujifunza siku hadi siku wakiwa UVCCM,” alisema Shaka.

Akizungumzia malalamiko ya uteuzi wa Jokate, Shaka alisema maneno yanayosambaa kwamba kiongozi huyo alilazimisha wajumbe wa kamati kulipitisha jina hilo si ya kweli na kwamba yana lengo la kuchafua jumuiya hiyo.

“Hakuna jina jingine lililokwenda kwenye kikao zaidi ya la Jokate na wajumbe wote walilipitisha kwa furaha, hizo zinazotolewa ni propaganda tu na hazina nia njema na UVCCM,” alisema Shaka.

 Mbali na Jokate, wengine walioteuliwa ni Dorice Obeid ambaye amekuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi, Uwezeshaji na Fedha, Daniel Zenda (Idara ya Vyuo na Vyuo Vikuu), Mohammed Abdalla (Idara ya Oganaizesheni, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa) na Israel Sostenes (Idara ya Usalama na Maadili).

Wakati huo huo, Katibu wa Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jasson Rweikiza, ametoa ufafanuzi kuhusu kikao kinachotarajiwa kufanyika leo mjini Dodoma cha wabunge wa chama hicho.

Katika taarifa aliyoituma jana kwa vyombo vya habari, Rweikiza alitoa ufafanuzi kwamba kikao hicho hakijaitishwa na Rais Dk. John Magufuli bali Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye ndiye mwenyekiti wa wabunge wa CCM bungeni.

“Leo (juzi) kuna baadhi ya magazeti yameandika habari, kwamba Rais Magufuli ameitisha kikao cha wabunge wa CCM. Inadaiwa ni kufuatia ujumbe wangu kwa wabunge wa CCM kuwa tutakuwa na kikao na Rais atakuwepo, habari hiyo si sahihi,” alisema.

Hata hivyo, Rweikiza alikiri kutuma ujumbe kwa wabunge wote wa CCM akiwaarifu juu ya kikao hicho na kuwataka wote wahudhurie.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,628FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles