Shahidi wa pili kesi ya kina Shamim aeleza alivyoshuhudia vielelezo vikifungwa

0
756

Kulwa Mzee -Dar es salaam

MFANYA usafi jengo la Utumishi, Kelvin Charles (22), ameieleza Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi jinsi yeye pamoja na mshtakiwa Shamim Mwasha na mumewe walivyoshuhudia vielelezo vikifungwa ili kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

Charles ambaye ni shahidi wa pili katika kesi hiyo ya kukutwa na dawa za kulevya inayomkabili Shamim na mumewe, alidai hayo jana katika mahakama hiyo.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula mbele ya Jaji Elinaza Luvanda, Charles alidai Inspekta Johari alimfuata katika eneo lake la kazi ili akashuhudie ufungaji wa vielelezo hivyo Mei 2 mwaka jana.

Alidai unga uliokuwa umefungwa kwenye kitambaa cheupe, mwingine katika vikopo vya plastiki ulikuwa mweupe na mwingine unga wa kaki ambao ulipewa majina A ambao awali ulidaiwa kuwa gramu 232.70, B gramu 68.52, C gramu 8.27,  D gramu 42.70 na E gramu 7.

Shahidi huyo alidai bahasha zote zilifungwa kwa lakiri na yeye pamoja na washtakiwa wote wawili walisaini nje ya bahasha hizo zilizofungwa.

Akihojiwa na wakili Juma Nassoro, alidai yeye ni shahidi huru, aliwafahamu washtakiwa siku ya ufungaji wa vielelezo hivyo na walishiriki pamoja, na wote walisaini juu ya vielelezo hivyo ambavyo baada ya kufungwa walifahamishwa vinapelekwa kwa Mkemia kwa uchunguzi zaidi.

Mawakili wengine wa utetezi ni Josephat Mabula na Hajra Mungula.

Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Abdul Nsembo.

Washtakiwa hao wanadaiwa Mei mosi mwaka jana walikutwa na dawa za kulevya nyumbani kwa Nsembo maeneo ya Mbezi Beach.

Washtakiwa wanaendelea kusota rumande hadi kesi hiyo itakapomalizika sababu hawaruhusiwi kupata dhamana kisheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here