33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Shahidi kesi ya kina Mbowe apumua

KULWA MZEE-DAR ES SALAAM

SHAHIDI wa sita wa Jamhuri, Koplo Charles, amemaliza kutoa ushahidi akidai maneno yaliyotamkwa na baadhi ya washtakiwa, hawezi kujua kama ni kosa ama si kosa, mwenye kujua hayo ni mpelelezi wa kesi.

Koplo Charles aliyehojiwa na upande wa utetezi kwa siku mbili, alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Jackline Nyantori katika ushahidi wake wakati akihojiwa na Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alidai mshtakiwa John Mnyika (Mbunge wa Kibamba) hakufanya mkusanyiko usio halali kwa sababu aliamini hivyo, kwani baada ya kuondoka hakujua kilichotokea nyuma yake.

Alidai maneno kuchinja, patachimbika, kubeba majeneza hawezi kujua yalikuwa na athari kiasi gani, anayeweza kujua ni mpelelezi.

Shahidi anadai ghasia zilimfanya ashindwe kuendelea kuchukua picha akihofia vifaa vya thamani alivyokuwa navyo na ingekuwa hatari kwa maisha yake.

Alipomaliza kutoa ushahidi, akaingia shahidi wa saba ambaye ni Ofisa Uchaguzi Manispaa ya Kinondoni, Victoria Mwihenge (34).

SHAHIDI WA SABA

Mwihenge alidai kuwa Januari mwaka jana, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), alitangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Kinondoni.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, shahidi huyo alidai taarifa ya tume ilielekeza kwamba uchaguzi huo unapaswa kufanyika Februari 17, 2018.

Alidai baada ya taarifa hiyo, Msimamizi wa Uchaguzi manispaa hiyo ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, aliitisha kikao cha wadau wa vyama vya siasa vilivyosajiliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Alidai jumla ya vyama vya siasa 19 vikiwakilishwa na mwenyekiti na katibu wa wilaya vilishiriki kikao hicho ambacho lengo lake lilikuwa kuwajulisha tarehe ya uchaguzi, siku ya kufanya uteuzi wa wagombea ubunge na kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo.

“Miongoni mwa vyama vilivyoshiriki katika kikao hicho ni Chadema, CCM, Ada Thadea, AFP, CUF, UND, Demokrasia Makini, TLP na NRA.

“Viongozi wa vyama hivi tuliwataarifu kuhusu uwepo wa Uchaguzi wa Mbunge Jimbo la Kinondoni na ushiriki wao katika kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika,” alidai Mwihenge na kuomba kesi iahirishwe anaenda kuonana na daktari. Kesi iliahirishwa na itaendelea leo.

Katika kesi ya msingi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake wanadaiwa kuwa kati ya Februari Mosi na Februari 16, mwaka huu wakiwa Kinondoni, Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama na wengine ambao hawapo mahakamani, kutenda kosa la jinai ikiwamo kuendelea na mkusanyiko isivyo halali na kusababisha chuki na uchochezi wa uasi.

Ilidaiwa kuwa Februari 16, mwaka huu, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, Ester Bulaya ambaye ni Mbunge wa Bunda, alishawishi wakazi wa eneo hilo kutenda kosa la jinai kwa kufanya maandamano yenye vurugu.

Ilidaiwa Februari 16, mwaka huu barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni, Wilaya ya Kinondoni kwa pamoja washtakiwa na wenzao zaidi ya 12, walifanya mkusanyiko na kukaidi amri halali ya ofisa wa Jeshi la Polisi, Gerald Ngiichi na kusababisha kifo cha Akwilina Akwiline na askari polisi wawili; Konstebo Fikiri na Koplo Rahim Msangi kujeruhiwa.

Ilidaiwa siku ya tukio la kwanza na la pili, katika viwanja vya Buibui vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam, katika mkutano wa hadhara, mshtakiwa John Heche ambaye ni Mbunge wa Tarime Vijijini, alitoa lugha ya kuchochea chuki akitamka maneno; “Kesho patachimbika upumbavu ambao unafanywa kwenye nchi hii… wizi unaofanywa na Serikali ya awamu ya tano… watu wanapotea… watu wanauawa wanaokotwa kwenye mitaro lazima ukome… “.

Imedaiwa kuwa maneno hayo yalielekea kuleta chuki kati ya Serikali na Watanzania.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Katibu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles