32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 1, 2023

Contact us: [email protected]

Sh milioni 302 zakusanywa mashindano ya baiskeli

NA MWANDISHI WETUZAIDI ya Sh milioni 302.6 zimekusanywa katika kilele cha mashindano ya baiskeli ya ACACIA Imara Pamoja Cycle Challenge, ambayo lengo kuu ni kuchangisha fedha kutekeleza miradi itakayoboresha upatikanaji wa elimu kwa jamii zinazozunguka migodi kampuni Acacia kanda ya ziwa.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Kampuni ya Uchimbaji Madini –ACACIA kwa kushirikiana na Taasisi binafsi kutoka nchini Canada (CanEducate), yameshirikisha wanaume katika mbio za Kilomita 140 na wanawake km 87.

Mzunguko wa mashindano hayo yaliyofanyika leo jijini Mwanza ulianza na kumalizikia katika Hoteli ya Malaika Resort kwa kupitia maeneo ya Kibandani, Igombe, Sangabuye, Kayenze, Nyanguge na Usagara, Buhongwa.

Akizungumza katika kilele cha mashindano hayo, Meneja Uboreshaji tija wa kampuni hiyo, Janet Reuben alisema jumla ya washiriki 211 wameshiriki katika mbio hizo.

Alisema kila mwaka ACACIA imekua ikidhamini mashindano ya baiskeli ya kanda ya ziwa chini ya jina la Acacia Tufanikiwe Pamoja Cycle Challenge.

“Hata hivyo, mwaka huu mashindano hayo yamepewa jina Acacia Imara Pamoja Cycle Challenge ili kuakisi dira mpya ya kampuni inayolenga kujenga mahusiano imara zaidi na jamii na wadau wetu. “Pia uamuzi huu wa kubadili jina unatokana na kuongezeka kwa kipengele cha uchangishaji fedha katika mashindano ya mwaka huu kwa ajili ya kusaidia sekta ya elimu.

“Kwa niaba ya uongozi wa Acacia kwa kupitia migodi yetu ya dhahabu ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara, wadau wetu CanEducate na kamati ya maandalizi, nipende kuwashukuru kwa uwepo wenu leo, pia nawapongeza washindi na washiriki wote kwa kumaliza mbio hizi salama,” alisema.

Alisema uamuzi wa kuendelea kujihusisha na mbio za baiskeli umechangiwa na mapenzi makubwa ambayo watu wa kanda ya ziwa wanayo juu ya mchezo huo.

“Mpango huo pia unatoa kipaumbele katika kuhakikisha jamii zetu – hasa watoto wa kike – wanapata elimu bora kama njia moja wapo ya kujikwamua na umaskini na kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuinua uchumi na hali za maisha ya watanzania kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Maendeleo 2025.

Aliongeza kuwa fedha hizo zitaelekezwa katika udhamini wa wanafunzi unaofanyika kati ya Acacia na CanEducate.

Aidha, Rais wa Chama Waendesha Baiskeli nchini, Godfrey Mhagama alimtangaza mshindi wa kwanza katika mbio hizo kwa upande wa wanaume kuwa ni Masunga Duba aliyejinyakulia Sh milioni 1.2, wapili Gerald Konnda (sh 900,000) na watatu Mungu Ataleta (Sh 500,000).

“Kwa upande wa wanawake mshindi ni Laurencia Luzuba (Sh milioni moja) na wa pili Tatu Malulu (Sh 800,000),” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles