27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

Sh bilioni 125 kuimarisha sekta afya ngazi ya msingi

Na Mwandishi wetu -Dodoma

SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendelo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wanaochangia sekta ya afya kupitia Mfuko wa Afya wa Pamoja (Health Basket Fund) imeridhia kuweka saini hati ya Sh bilioni 125.69 kuimarisha huduma za afya katika ngazi ya msingi nchini. 

Akizungumza wakati wa kuidhinisha makubaliano hayo,  Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Mabula Mchembe alisema lengo kuu la mfuko huo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999 ni kuimarisha huduma za afya katika ngazi ya msingi (halmashauri) zote nchini. 

Alisema katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2020/21  wadau nane watachangia Dola za Marekani milioni 53.84 sawa na Sh bilioni 125.69 kwa kipaumbele cha kuimarisha huduma za afya katika vituo vya afya kwenye halmashauri zote 184 nchini.

“Sh bilioni 105.32  zitatumika kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za afya katika vituo vya afya vipatavyo 5,533 kwenye halmashauri zote 184 nchini ikiwa ni pamoja na ununuzi wa dawa, vifaa na vifaa tiba, uendeshaji wa vituo, ukarabati mdogo na huduma za chanjo na vikoba.

 “Fedha hizo zitapelekwa moja kwa moja vituoni kwa utaratibu wa ‘Direct Health Facility Financing,” alisema Profesa Mchembe.

Aidha, Profesa Mchembe alisema Sh bilioni 4.29 zitatumika kuziwezesha timu za afya za mikoa 26 kufanya ufuatiliaji na usimamizi shirikishi katika halmashauri zote nchini na Sh bilioni 2.09 zitawezesha Ofisi ya Rais– Tamisemi kusimamia na kutoa msaada wa kitalaamu katika halmashauri na mikoa yote nchini. 

Alisema Sh bilioni 5.13 zitawezesha Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutekeleza masuala ya sera, mikakati na miongozo kuhakikisha huduma za afya zinatolewa kwa kiwango na ubora stahiki na Sh bilioni 8.86 zitakuwa kwa ajili ya kutekeleza maeneo mengine ya kipaumbele katika sekta.

“Vipaumbele tulivyoidhinisha na kamati ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu 620 wa dawa za usingizi, kununua mashine za kisasa za kutolea dawa za usingizi katika vituo vya afya ngazi ya halmashauri na kufanya ukarabati mkubwa katika vyuo vinne vya kutolea mafunzo ya wataalamu wa afya,” alisema Profesa Mchembe.

Alitaja maeneo mengine ya kipaumbele yaliyoidhinishwa na Kamati Kuu ya mfuko huo kuwa ni kuhuisha Mkataba wa Makubaliano (MOU) baina ya pande zote mbili kwa kipindi cha 2021 – 2026, kununua mashine za kutolea dawa za usingizi katika vituo vya kutolea huduma za afya pamoja na kuvijengea uwezo vituo vya afya katika kusimamia na kutumia fedha kwa kuzingatia miongozo na taratibu mbalimbali. 

Maazimio ya uwekaji saini hati hiyo yamefanyika kwenye ofisi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iliyoko mji wa Serikali Mtumba.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wataalamu kutoka Wizara ya  Afya, Wizara ya Fedha na Mipango, Ofisi ya Rais  Tamisemi, Bohari ya Dawa (MSD) na wadau wa maendeleo wanaochangia mfuko huo kutoka Canada, Denmark, Koica, Ireland, Uswisi, Unicef, UNFPA na Benki ya Dunia walioshiriki kwa njia ya ‘video conference’. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles