Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
SHIRIKAl la lisilo la kiserikali la Helvetas, limetoa Sh bilioni 1.15 na Chama cha walimu Tanzania (CWT) Sh. milioni 300, lengo likiwa kusaidia mradi wa SITT unaolenga kuboresha mbinu za walimu kufundisha.
Meneja wa mradi huo, Donatian Marusu, alisema kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya kutimiza jukumu la kuhakikisha mpango wa kusaidia walimu kitaaluma unakuwa endelevu.
Marusu alisema kupitia mradi huo, zaidi ya walimu 285 na walimu wakuu 95 kutoka mikoa ya kati na walimu 130 na walimu wakuu 130 kutoka mikoa ya kaskazini watanufaika.
Pia alisema zaidi ya wanafunzi 49,000 katika mikoa ya kati na 61,000 kutoka mikoa ya kaskazini watanufaika na mafunzo, ikiwa ni pamoja na kupatiwa vitabu vya hisabati na sayansi ya mazingira.
“Mgeni rasmi tunayo furaha kubwa kukukaribisha katika mkutano huu wa wadau wa elimu kwa ajili ya kuutambulisha mradi wa Inclusive School based In-services Teacher Training ambao kwa kifupi hujulikana kama Inclusive SITT, ambao utatekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga,” alisema Marusu.
Alisema mradi huo umekuja kutokana na ombi la wadau kutaka kupanua kutoka mikoa ya kaskazini – Arusha, Manyara na Kilimanjaro na kuongeza mingine minne.
“Mikoa ya awamu hii ni Dodoma, Singida, Tabora na Shinyanga na wilaya zitakazonufaika ni Chemba, Kondoa Mji, Mpwapwa, Iramba, Shinyanga Mji, Tabora Manispaa, Urambo na Nzega na utatekelezwa kupitia wakufunzi kutoka vyuo vya ualimu sita ambavyo ni Bustani, Mpwapwa, Kinampanda, Shinyanga, Tabora na Ndala,” alisema Marusu.
Alisema wakufunzi wa hisabati 24 kutoka vyuo hivyo, watapatiwa mafunzo ya mbinu na ufundishaji somo hilo na watakabidhiwa jukumu la kutoa mafunzo kwa walimu walio kwenye mradi huo.
“Kutokana na jitihada zilizofanyika katika awamu ya kwanza ya mradi, kumekuwepo na mafanikio kama vile ongezeko la ufaulu kwa wahitimu wa elimu ya msingi kwenye masomo ya hisabati, kiingereza na maarifa ya jamii,” alieleza Marusu.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dk. Avemaria Semakafu, aliwataka walimu waliopata nafasi katika mradi huo kuwa chachu ya mafanikio kwenye maeneo yao.
“Tatizo kubwa tulilonalo ni changamoto ya mbinu za kufundishia, programu hii ikasaidie katika kuboresha ufundishaji katika shule zetu ili kuboresha utoaji wa elimu nchini,” alisema Dk. Semakafu.