25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Serukamba atonesha vidonda Escrow, Tokomeza

peter-serukambaKhamis Mkotya na Arodia Peter, Dodoma
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), ametonesha vidonda vya ufisadi baada ya kuzungumzia ripoti ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue iliyowasafisha baadhi ya watendaji serikalini waliohusika katika kashfa ya Escrow.

Serukamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, alishangazwa na taarifa hiyo kuwasafisha baadhi ya watu waliohusishwa katika kashfa hiyo na kuwaacha wengine, jambo ambalo alisema ni ubaguzi.

Kauli hiyo aliitoa bungeni mjini Dodoma jana alipokuwa akichangia Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoiwasilisha bungeni juzi akiomba Sh trilioni 5 kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016.

Katika mchango wake, Serukamba alisema ni vizuri Bunge likaitaka Serikali itangaze kuwa wote waliohusishwa katika kashfa hiyo nao ni wasafi.

Alisema haoni mantiki kwa Serikali kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliackim Maswi na Waziri Profesa Sospeter Muhongo na kuwaacha wengine waliowajibika pamoja.

Serukamba alisema kwa kuwa Serikali imewasafisha viongozi hao ni wazi kuwa muamala uliofanyika wa uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow ni halali.

Mbunge huyo alisema ili kutenda haki kwa watu wote ni vema wanasiasa wengine waliojiuzulu nyadhifa zao na kuwajibishwa kwa Azimio la Bunge warejeshwe katika nyadhifa zao.

Waliopoteza nyadhifa zao kutokana na kashfa ya Escrow ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba, William Ngeleja.

“Kuhusu suala la Escrow, juzi Katibu Mkuu Kiongozi alitoa ripoti baada ya uchunguzi kufanyika ripoti ikasema katibu mkuu wake na waziri wake ni safi maana yake mwamala ule ni safi.
“Kama mwamala ule ni safi, katibu ni safi waziri ni safi, Chenge anakuwaje mchafu? Tibaijuka anakuwaje mchafu? Ngeleja anakuwaje mchafu? Mliowapeleka mahakamani wanakuwaje wachafu? Haiwezekani tuache hizi ni style za zamani.
“Bunge lako linadhalilishwa watu walidanganya watu walileta document (nyaraka) feki wanatetewa, Tibaijuka tulimhukumu kwa nini? Ina maana kwa Serikali hii kuna watu ni wazuri na wengine ni wabaya tuambieni. Nataka waziri mkuu aje atuambie usafi wa hawa watu ni nini.

“Jingine mheshimiwa spika ni suala la Tokomeza, mmefanya vizuri sana, mheshimiwa spika tuliomba ripoti ya Tokomeza hawakuleta na kama Serikali mmesema mawaziri wale ni safi naomba muwarudishe katika wizara zao.

“Kule Kenya kipindi fulani Waziri wa Fedha alituhumiwa kwamba amekula rushwa akajiuzulu, Mwai Kibaki (rais mstaafu) akaunda tume ya judicial (tume ya kimahakama) kama mlivyounda kwenye Tokomeza, ripoti ilipotoka ilionyesha kuwa Waziri wa Fedha, Amos Kimunya hana kosa lolote, rais alimteua kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

“Mnapoamua kuchukua hizi njia za juu za good governance (utawala bora) msiishie nusu, haiwezekani muishie kwenye nusu, tukiamua kuchunguza na tukabaini kuwa hawakukosea tunawarudisha kwenye nafasi zao, ndiyo matakwa ya good governance (utawala bora). Tuache usanii hapa kwenye hili jambo.

“Kuna watu hapa Maige alituhumiwa kuwa alisafirisha wale wanyama twiga kwenda nje, muundieni tume ili tuone kweli kama ni yeye ndiye alikwenda kwenye ndege kuwaingiza pundamilia ili na yeye mumsafishe mbona mnasafisha watu nusu, hii ni nini?
“Akina Ngeleja hapa akina Mkulo waundieni tume wote tujue kama walikosea. Haiwezekani muumize wachache mimi katika hili hapana kama kuna jambo linaniumiza ni injustice, haiwezikani tuwe na Serikali ya double standard (ndumilakuwili).

“Walijiuzulu akina Karamagi (aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini) hapa akina Msabaha (aliyekuwa Waziri wa Afrika Mashariki), waziri mkuu (Edward Lowassa). Kwa nini hamkuunda judicial inquiry (tume)?” alisema na kuhoji Serukamba.

Mbunge huyo alisema inaweza kuwa ndiyo njia nzuri za utawala bora kwa mtu aliyejiuzulu kuundiwa tume kujua kama kweli alikosea arudishwe katika nafasi yake.

“Suala hili la Escrow mheshimiwa spika lazima akina Chenge nao wasafishwe, vinginevyo mniambie na hawa mliowasafisha ni wachafu. Mnatumia nguvu nyingi kuwasafisha lakini mnafanyaje nusu? Au wengine mna ajenda nao?

“Hebu tuambieni kama kuna ajenda, hapa akina Mwambalaswa walivuliwa uenyekiti wa kamati na wenyewe semeni kwamba hawakukosea kwa nini muishie nusu?
“Hatuwezi kunyamaza tuache uonevu kwa watu haiwezekani, kuna watu ni wema na wengine ni wabaya haiwezekani. Hiki si chama tunachokijua wote. Werema (aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali) aliondoka kwa sababu gani, maana kama mnasema mwamala ni safi waliosimamia wote ni safi wengine ni wachafu. Kuna watu Ikulu nao walituhumiwa lakini bado wapo ofisini sasa Werema mlimuondolea nini uanasheria wake?” alisema.

Baada ya kumaliza kuchangia, Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM) alinyanyuka katika kiti chake na kwenda kumpa mkono Serukamba na baadaye alitoa ndani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles