32.2 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali yazungumzia miaka minne ya JPM

Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam

SERIKALI imesema imeweka mifumo imara ya kitaasisi na kisheria inayohakiki miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano, kuhakikisha inaendelea kuleta manufaa endelevu kwa faida ya Watanzania wote.

Hayo yamebainishwa jana Dar es Salaam na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi wakati wa mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akizungumzia tathmini ya miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli.

Alisema ipo miradi mikubwa ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, hivyo ili iwe na matokeo chanya, Serikali imeweka mifumo imara ya kitaasisi na kisheria kulinda mafanikio hayo, hata baada ya Serikali ya awamu ya tano kumaliza muda wake.

“Tanzania kwa sasa ndani ya kipindi kifupi cha miaka minne tumeweza kufanya mambo mengi, ikiwemo kukabiliana na rushwa, kwa sasa tumeunda mahakama maalumu ya mafisadi ambayo tayari imesikiliza kesi zaidi ya 50,” alisema Dk. Abbasi.

Alisema ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli, Serikali imenunua ndege jambo ambalo awali lilikuwa na ugumu katika utekelezaji wake.

“Jambo jingine ni suala la kuhamia Dodoma. Jambo hili kwa sasa si ndoto tena, asilimia 90 ya watumishi wa Serikali katika wizara na baadhi ya idara, taasisi na wakala za Serikali wamehamia Dodoma na Serikali imeweka msingi wa kisheria wa kuitangaza Dodoma kuwa ni makao makuu ya Serikali,” alisema Dk. Abbasi.

Alisema ili maendeleo hayo yazidi kuleta manufaa kwa vizazi vijavyo, Watanzania hawana budi kuwa wazalendo na walinzi wa mali za umma na kutoa taarifa katika mamlaka za Serikali kuhusu uharibifu na ubadhirifu unaofanywa na mtu au kikundi chochote katika jamii.

Dk. Abbasi alisema Serikali kupitia ushirikiano wake na wananchi imetekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya, maji, elimu na barabara, ambayo imeendelea kuwagusa wananchi wengi zaidi hususani wa kipato cha chini.

Alisema Serikali inatekeleza miradi ya maji 1,600 nchi nzima, ikiwemo 300 inayotekelezwa maeneo ya vijijini na Sh bilioni 700 zimetumika kuitekeleza.

Kuhusu sekta ya afya, Dk. Abbasi alisema Serikali kwa sasa imeiimarisha kwani Tanzania imekuwa nchi mfadhili kwa kuweza kufanya huduma za kibingwa ambazo zilikuwa zikifanyika nje ya nchi na kuifanya Serikali kupoteza kiasi kikubwa cha fedha.

“Ndani ya kipindi cha miaka minne, Serikali imeweza kuongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka Sh bilioni 31 mwaka 2014/15 hadi bilioni 270, pia kuajiri waganga wataalamu zaidi ya 6,000 wanaohudumia wagonjwa katika hospitali zetu za mikoa, wilaya, vituo vya afya katika kata na zahanati katika maeneo ya vijijini,” alisema Dk. Abbasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles