25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yazindua kampeni kutokemeza malaria

Na LEONARD MANG’OHA -KIBAHA

SERIKALI kwa kushirikiana na taasisi isiyo ya kiserikali ya Kumekucha Tanzania, imezindua kampeni ya kuhamasisha jamii kutokomeza mazalia ya mbu wanaosababisha ugonjwa wa malaria kwa kutumia dawa inayozalishwa na kiwanda cha kutengeneza viuadudu (TBPL) cha Kibaha mkoani Pwani.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda hicho, Profesa Madundo Mtambo, wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha mkoani Pwani jana.

Alisema lengo la kampeni hiyo ni kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kushiriki kutokomeza mazalia ya mbu kwa mafanikio na hatimaye kutokomeza kabisa malaria nchini.

Profesa Madundo alisema tayari kiwanda hicho kimeanza uzalishaji wa viuatilifu kwa magonjwa yanayoshambulia zao la pamba kama ilivyoagizwa na Serikali.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Leonard Subi, alisema ripoti ya dunia ya mwaka 2018 kulikuwa na maambukizi ya malaria milioni 219 na vifo 435,000.

Alisema asilimia 91 ya nchi zinazoathirika zaidi na malaria duniani ziko Bara la Afrika, ambapo nchi 10 zenye viwango vya juu vya maambukizi ya malaria zinatoka bara hilo, ikiwamo Tanzania.

Alisema ugonjwa huo umepungua nchini kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi 7.3 mwaka 2017, huku vifo vinavyosababishwa na ugonjwa huo pia vikipungua kutoka 6,300 mwaka 2015 hadi 2,079 mwaka jana.

Dk. Subi alisema kupungua kwa ugonjwa huo kunatokana na uongozi imara wa Serikali, kuongezwa kwa bajeti ya dawa na kuimarika kwa utoaji wa huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini na matumizi sahihi ya takwimu katika kupambana na ugonjwa huo.

Alisema tafiti zinaonyesha kuwa kiasi cha watu milioni 50 wako katika hatari ya kuambukizwa malaria hapa nchini na kwamba makundi ya watoto chini ya umri wa miaka mitano na wanawake wajawazito ndio wako katika hatari zaidi.

Kuhusu matumizi ya dawa ya viuadudu inayotengenezwa na kiwanda cha kutengeneza viuadudu cha Kibaha mkoa wa Pwani, alisema kuwa dawa hiyo imeonyesha mafanikio makubwa kwa kiua viluwiluwi kwa zaidi ya asilimia 96.

Alisema kuwa ili dawa hiyo ilete matokeo mazuri inahitaji ushirikiano wa pamoja na kwamba hategemei kuona mtu mmoja akinyunyiza dawa hiyo kwenye eneo lake, badala yake wananchi wanaweza kuungana kuyatambua mazalia ya mbu na kuyaangamiza.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kumechuka Tanzania, Jackson Cyprian, alisema kupitia kampeni hiyo ambayo imeanza kutekelezwa baadhi ya mikoa kuhamasisha na kusajili mawakala ili kuwezesha dawa hiyo kwa urahisi ndani ya kipindi cha siku 120.

Alisema bado uelewa wa wananchi kuhusu kiwanda cha TBPL ni mdogo na kwamba hata wakazi wa Kibaha wenyewe wanaamini kiwanda hicho ni mali ya wawekezaji kutoka Cuba na kwamba dawa zinazozaliwa ni kwa ajili ya matajiri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles