33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yazima jaribio la mapinduzi Gabon

LIBREVILLE, GABON


JARIBIO la wanajeshi wa ngazi za chini kuipindua Serikali ya Gabon limezimwa na vikosi vitiifu kwa Rais Ali Omar Bongo aliye matibabuni nchini Morocco


Kwa mujibu wa Waziri wa Mawasiliano Gabon, Guy-Bertrand Mapangou wanajeshi wanne kati ya watano waliohusika katika jaribio hilo jana asubuhi wamekamatwa na aliyebakia anaendelea kusakwa.


“Hali ni tulivu. Polisi wanaolinda makao makuu ya vituo vya redio na televisheni wamerejea na kuchukua udhibiti wa eneo lote, kwa hivyo kila kitu kiko katika hali ya kawaida,” alisema.


“Walikuwa watano. Wanne wamekamatwa na mmoja yu mafichoni na atakamatwa saa chache zijazo,” alisema Mapangou.
Awali mapema jana kundi la wanajeshi waasi lilitangaza kuendesha mapinduzi ya serikali katika taifa hilo la Afrika Magharibi.


Likiwa limechukua udhibiti wa kituo cha redio na kile cha televisheni saa 10 alfajiri sawa na saa 12 asubuhi za Afrika Mashariki, lilieleza uwapo wa hali ya wasiwasi kuhusu uwezo wa Rais Bongo kuongoza nchi hiyo.


Ujumbe wa kundi hilo ulitumwa na mtu aliyejitambulisha kama naibu kamanda wa kikosi cha ulinzi wa rais na mkuu wa kundi liitwalo Vuguvugu la Vijana Wazalendo Jeshini na na katika Vikosi vya Usalama vya Gabon, Luteni Kelly Ondo Obiang.


Obiang alidai wamepania kurejesha demokrasia na kueleza mpango wa kuunda Baraza la Taifa la Ukombozi kurejesha utawala wa kiraia tofauti ulio tofauti na kurithishana madaraka kama wa familia ya Bongo.


Aidha alikosoa hotuba ya Mwaka Mpya iliyotolewa na Rais Bongo Desemba,31 mwaka jana, akisema mawazo katika hotuba hiyo hayakutiririka vyema na sauti yake ilikuwa dhaifu.


Obiang alisema hotuba ya Rais Bongo ilithibitisha mashaka yao kuhusu uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake.
Katika hotuba hiyo, Bongo alikiri kuwa anakumbwa na matatizo ya kiafya lakini alisema anapata nafuu.


Vuguvugu hilo lilikuwa limetoa wito kwa vijana kutoka vikosi vyote vya usalama pamoja na vijana raia Gabon kujiunga nao.


“Ile siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa sasa imefika. Jeshi limeamua kuungana na umma kuiokoa Gabon dhidi ya machafuko. Kama unakula, acha; kama unakunywa, acha; kama umelala, amka.

Muamshe jirani yako. Simameni pamoja na ingieni mitaani muidhibiti hali,” alisema kwenye redio.
Aidha aliwataka wananchi washikilie majengo ya umma na viwanja vya ndege kote nchini.


Haya yalijiri wakati Rais Bongo akiendelea kutibiwa katika makazi yake binafsi kwenye mji mkuu wa Morocco, Rabat.


Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 59 hajarejea nchini Gabon tangu alipougua ghafla Oktoba 24 mwaka jana akiwa nchini Saudi Arabia.


Familia ya Bongo imelitawala taifa hilo lenye utajiri wa mafuta kwa miongo minne sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles