Yatoa onyo kwa watakaokaidi kutopewa leseni
Na Clara Matimo, Mwanza
Serikali imewataka wafanyabiashara wa madini Mkoani Mwanza walio na ofisi katika jengo la Rock City Mall, kuhamia kwenye soko jipya la madini lililopo Kata ya pasiansi Wilaya ya Ilemela kilipo kiwanda cha kusafisha dhahabu Mwanza Precious Metal Refinery.
Pia imesema baada ya kukamilisha usajili wa viwanda vya kusafisha dhahabu vilivyopo mikoa ya Mwanza, Geita na Dodoma itazuia usafirishaji wa dhahabu ambayo haijasafishwa kwenda nje ya nchi.
Agizo hilo limetolewa Oktoba 11, jijini hapa na Waziri wa Madini, Dk. Doto Biteko, wakati akizungumza na wafanyabiashara pamoja na wachimbaji wadogo wa madini Mkoani Mwanza ili kubaini changamoto zao.
Alisema wafanyabiashara watakaokaidi kuhamia katika soko hilo wizara hiyo haitashughulika na maombi yao ya leseni ambazo zimekwisha muda wake kwa kuwa serikali imetumia gharama kubwa kuhakikisha ujenzi wa soko hilo unakamilika lengo likiwa ni kuwawekea mazingira bor na rafiki.
“ Mimi ninauwezo wa kusema muhame ndani ya wiki mbili zijazo lakini sitaki kuonekana dikteta, dealers wote simameni niwaone ambaye anasema yeye hawezi kwenda kwenye hilo soko jipya aniambie hapa hapa ili tusihangaishane na maombi yake ya leseni tutamtafutia eneo lingine aende.
“Nyie wenyewe mliniambia moja ya changamoto ni gharama kubwa hapo rock city mall mnalipa Sh milioni tano hadi tisa kwa mwaka , nia ya serikali ni kuwatua mzigo huko tunakowapeleka ni jengo la serikali mtalipa umeme na maji tu hamtalipa gharama zingine zozote na mazingira ni rafiki mnataka tuwafanyie nini?Alihoji ” Biteko.
Alisema nia ya serikali ni kuona wachimbaji madini wanafanya shughuli zao kwa uhuru bila kuonewa wala kunyanyaswa na wao walipe kodi stahiki ndiyo maana iko mstali wa mbele kuwatatulia changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo.
Akizungumzia kuzuia kusafirisha nje dhahabu ambayo haijasafishwa, Waziri Biteko alisema “Tukikamilisha usajili yaani certification tutasafirisha tu nje ya nchi dhahabu ambayo imeishasafishwa kwa sababu mimi nitakuwa waziri wa ajabu sana nina feed refinery za wengine halafu tuna refinery humu ndani ambazo sisi wenyewe tumevutia mitaji watu wamewekeza halafu hawapati malighafi,”alisema.
Awali akisoma hotuba ya wachimbaji mbele ya Waziri Biteko, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mwanza (Mwarema) Richard Seni, alitaja miongoni mwa changamoto zinazowakabili kuwa ni pamoja na ukubwa wa tozo za halamshauri ambazo zinazidi mrabaha na zinatozwa kwenye malighafi ambapo alipendekeza kuondolewa tozo zote zinazokinzana na sheria ya madini ibaki asilimia 0.3 pekee ambayo nayo itozwe kwenye madini.
Vile vile aliiomba serikali maeneo yote ya rush yapatiwe leseni yakiwemo Ghatta Mining Group, Mlimani Mining Group lengo ni kupunguza migogoro lakini pia kuwafanya wachimbaji kuwekeza mitaji yao kwa uhuru na uhakika kitendo kitakachowafanya kukopesheka kwa urahisi zaidi.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dk. Angeline Mabula, alisema uwepo wa kiwanda hicho jimboni humo kimewezesha kutoa ajira kwa vijana inayowawezesha kujikimu kimaisha.