Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Serikali imewataka Watanzania kuzingatia na kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi walizopo ili kulinda taswira nzuri ya nchi yao.
Rai hiyo imetolewa leo Januari 24, 2023 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Stergomena Tax alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelezea taarifa juu ya kifo cha Mtanzania, Nemes Tarimo, mtanzania aliyefariki dunia nchini Urusi.
Dk. Tax amefafanua kuwa kwa mujibu wa sheria za Tanzania, Mtanzania yeyote haruhusiwi kujiunga na Jeshi la nchi yoyote duniani zaidi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kufuata taratibu zilizopo.
“Nitoe rai kwa watanzania kuhakikisha wanazingatia sheria kanuni na taratibu za nchi walizopo, na pia wawe mabalozi wazuri wa kulinda taswira ya Tanzania. Ikumbukwe kuwa kwa mujibu wa sheria zetu, Mtanzania yoyote haruhusiwi kujiunga na jeshi la nchi yoyote isipokuwa Jeshi la Tanzania na kufanya hivyo ni kuvunja sheria,” amesema Dk. Tax.
Dk. Tax amesema Mtanzania huyo alikwenda nchini Urusi mwaka 2020 kwa lengo la kujiunga na Chuo Kikuu cha Moscow Technological University (MIREA) kwa masomo ya Shahada ya Uzamili katika fani ya Business Informatics.
Ameongeza kuwa Mwezi Machi 2022, Mtanzania huyo alitiwa hatiani kwa kuhusika na vitendo vya uhalifu na kwa mujibu wa Sheria za Urusi alihukumiwa kifungo cha miaka saba (7) jela.
Waziri Tax ameongeza kuwa Bw. Tarimo akiwa gerezani alijiunga na kikundi cha kijeshi cha Urusi cha Wagner kwa ahadi ya kulipwa fedha na kuachiwa huru baada ya kumaliza muda wa kutumika vita na alifikwa na umauti akiwa nchini humo.
Dk. Tax amesema kuwa mwili wa marehemu umeondoka nchini Urusi Januari 24, 2023 na unatarajiwa kuwasili nchini muda wowote kuanzia sasa na kuongeza kuwa Serikali imekuwa ikiwasiliana na Serikali ya Urusi ili kuhakikisha mwili wa Marehemu Tarimo unarejeshwa nchini na kukabidhiwa kwa familia yake kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Waziri ametoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa na Watanzania kwa jumla kufuatia msiba huo.
Dk. Tax amewauhakikishia umma na Diaspora wa Kitanzania wakiwemo wanafunzi walioko masomoni duniani kote kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wakati wote.