27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAWAKATISHA TAMAA WABUNIFU UJENZI VIWANDA (2)

Na Gordon Kalulunga,

WAKATI nia ya kuwa nchi ya viwanda ikiwa tayari imetangazwa na Rais Dk. John Magufuli Novemba 20, mwaka 2015, Serikali inadaiwa kuwakatisha tamaa wabunifu wasio wasomi kuendeleza viwanda vidogo.

Pamoja na kuwepo kwa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) ambayo moja ya majukumu yake ni kutafuta, kutunza na kusambaza taarifa za sayansi na teknolojia na kuzikuza nchini, bado jitihada za utekelezwaji wa majukumu ya tume hiyo ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, hazijaonekana kwa wabunifu hao ambao wengi wao hawana elimu  za vyuo vikuu…….Endelea toka sehemu ya (1)

“Serikali wakitaka kunisomesha nipo tayari, lakini Jiji walisema hawana mfuko wa kusomesha wabunifu na TBS, nilipokwenda walinitaka niwe na kiwanda, jambo ambalo nimefanikiwa kununua uwanja na kujenga nyumba  yangu na ofisi na walinitaka nijenge sehemu ya mapokezi, ofisi, karakana, stoo na vyoo”

“Rais Magufuli ni safi lakini baadhi ya watendaji wake ni siasa tupu. Mimi nimethibitishwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia lakini anakuja injinia wa Jiji ananiambia kuwa nisitishe uzalishaji na kwamba nimpe kifaa akapime kisha niende kusoma na baadaye nikaombe kibali kwao cha  kuendeleza ubunifu wangu, yaani kutengeneza hizi nyaya za umeme,” anaeleza  Charles Antony Sanga huku akitikisa kichwa.

Kwa sasa anaeleza kuwa tayari ameajiri wafanyakazi wanne na bidhaa zake zinasambazwa katika maduka ya vifaa vya ujenzi na anauza kuanzia Sh 15,000 kwa  kifaa kimoja.

“Serikali itufute na kutuuliza tunawezaje kuboresha ujuzi wetu katika vifaa tunavyotengeneza badala ya kutukatisha tama, huku bidhaa za nje  ya nchi zikiingizwa nchini zikiwa hazina ubora na ndiyo maana kila kukicha dunia nzima inalalamikia milipuko majumbani na viwandani maana  waya zilizopo ndani ya Extension Cable za plastic hazina ubora, ni  ndogo sawa na waya wa kuchajia simu ya kiganjani,” anaeleza mbunifu  huyo.

Msindikaji wa Kahawa katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mtemi Miya, anasema changamoto nyingine ni mikopo kwa viwanda vidogo ambapo riba za taasisi za fedha ni kubwa na kwamba pia malipo mara mbili mbili ambayo  yanayotokana na taasisi za TFDA/OSHA/TBS yanakuwa kikwazo kwao.

“Masharti na vigezo vyao vingi vinafanana na malipo ni makubwa kwa vitu vinavyofanana. Hivyo basi, tunaiomba Serikali iangalie ni kwa  namna gani inaweza kuweka hivi vigezo na masharti pamoja ili yalipiwe kwa pamoja badala ya kuwa na taasisi zaidi ya moja kwa vigezo vile  vile na kuvilipia tofauti tofauti,” anaeleza Miya.

Anasema  ili kutimiza kauli mbiu ya kuwa nchi ya viwanda, wanapendekeza kuwa Serikali kwa kupitia Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage, kuzisisitiza halmashauri zote nchini kutenga bajeti  kwenye mfuko wa maendeleo ili kutangaza bidhaa zinazozalishwa na  viwanda vidogo katika kila halmashauri na kuwasaidia wajasiriamali  kuzifikia fursa zilizopo.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini (Sido) Prof. Sylvester Mpanju, anasema Shirika lake litaendelea kutoa elimu kwa wajasiriamali na kuendelea kuwafuata popote walipo kwa ajili ya kuendeleza viwanda hapa nchini.

Meneja wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Abel Mwakasonda, anakiri kuwa hawajawafikia wabunifu wengi  lakini ofisi yake inafanya kila liwezekanalo kutoa elimu kwa wajasiriamali wote, ikiwa ni pamoja na kuwahimiza kujitokeza ili waweze  kupatiwa elimu.

Alipoulizwa vigezo vya kupima ubora wa bidhaa zinazozalishwa  na wabunifu hao ambazo hazitakiwi kupelekwa katika maabara, alisema kuna njia wanazozitumia ikiwa ni pamoja na kukutanisha jopo la wabunifu nchini.

“Tunapokuwa tumewapata wabunifu kama hawa wahunzi, bidhaa zao hatuzipeleki maabara bali tunawakusanya wabunifu wabobezi ambao ndio wanakagua bidhaa hizo na wanaporidhika na wanatupatia majibu yanayotuwezesha kumpatia nembo ya TBS mbunifu husika au kumshauri zaidi ili aweze kukidhi viwango vya kupata nembo yetu,” anaeleza Mwakasonda.

Anasema wabunifu na wajasiriamali wengi ni waelewa hivyo jukumu la shirika lake ni kuendelea kutoa elimu zaidi kwa ajili ya kufikia uchumi wa kati kupitia viwanda.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven, anasema wabunifu hao wakisaidiwa ipasavyo wataweza kufanikisha azma ya Taifa kufikia lengo la uchumi wa kati.

Anasema kuna watu wanatengeneza mpaka viatu vya kijeshi kwa kutumia ngozi za mifugo yetu hapa nchini, hivyo hakuna sababu ya kutumia gharama kubwa kuagiza kutoka nje ya nchi badala yake wabunifu hao wanapaswa kuendelezwa.

“Huu ndio msingi wa viwanda ambavyo Mheshimiwa Rais wetu anazungumzia kwamba, ili tutoke tuanze na haya ambayo wenzetu wa Sido na wananchi wale ambao wapo tayari kutuonyesha hapo ndipo tutaweza kushika kasi.

Lakini tukifanya mzaha, tukadharau tukabeza… mimi sijawahi kuona mtoto anazaliwa saa ile ile na kumaliza chuo saa ile ile, lazima twende hatua kwa hatua na hatua zenyewe ni hizi,” alisema Zelothe Steven.

Akisoma risala kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, katika maonyesho ya wajasiriamali wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika mwishoni mwa Septemba mpaka mwanzoni mwa Oktoba mwaka jana, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla, alisema msukumo wa Serikali ya awamu ya tano ni kuwa na viwanda vya ndani.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles