27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatumia zaidi ya Bilioni 60 kujenga na kukarabati vivuko

*Kimo cha Rugezi –Kisorya kinachojengwa na Kampuni ya songoro Marine Transport Ltd boatyard

Na Clara Matimo, Mwanza

Imeelezwa kwamba  mwaka  huu wa fedha 2022/2023 serikali itatekeleza ujenzi na ukarabati wa miradi 32 ya vivuko  pamoja na miundombinu yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 60 lengo likiwa ni kuboresha na kutatua changmoto za usafiri na usafirishaji kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima akiweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa kivuko kipya cha Kisory –Rugezi katika karakana hiyo iliyopo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Hayo yamebainishwa Oktoba 18, 2022 na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme(Temesa), Mhandisi Lazaro Kilahala wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa ujenzi wa kivuko kipya cha Kisory Rugezi kinachojengwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Boatyard ya  mkoani Mwanza kwa gharama ya Sh bilioni 5.5.

Mhandisi Kilahala amefafanua kwamba  kati ya miradi hiyo miradi saba ambayo itagharimu Sh bilioni 33.2 ni ya ujenzi wa vivuko vipya ambavyo ni Kisorya –Rugezi, Bwiro- Bukondo, Nyakarilo-Kome, Mafia–Nyamisati na Ijinga- Kahangala hadi sasa viko katika hatua mbalimbali za ujenzi maana wamekwishasaini  mikataba na wakandarasi wamekwishalipwa malipo ya awali.

“Vivuko viwili ambavyo  ni Buyagu-Mbalika na Magogoni –Kigamboni viko kwenye hatua za manunuzi  pia mwaka huu wa fedha serikali itakarabati jumla ya vivuko 14 kwa gharama ya Sh bilioni 22.99 ambavyo ni  Mv Misungwi, Kazi, Musoma, Sabasaba, Tanga, Nyerere,  Magogoni, Mara, Kitunda, Kilombero  II, Ruhuhu, Old Ruvuvu, Kome II na ujenzi.

“Vilevile tutafanya ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya vivuko ikiwemo madaraj ya kusimamia na majengo ya abiria ambapo tutatekeleza jumla ya miradi 11 yenye thamani ya Sh bilioni 4.1 hivyo serikali  itatumia jumla ya Sh bilioni 60.3 kutekeleza ujenzi wa miradi hiyo yote ya vivuko ambayo tayari mikataba imesainiwa na kazi inaendelea,”amesema Mhandisi Kilahala na kuongeza:

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima alipotembelea maeneo mbalimbali katika karakana ya Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Boatyard baada ya kuzindua ujenzi wa kivuko kipya cha Kisory –Rugezi.

“Tunaishukuru sana serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kutuwezesha kifedha kuweza kutekelza miradi hiyo ambayo lengo lake ni kutatua changamoto za wananchi nasi  kama watendaji tunaahidi kufanya kazi kwa weledi na jitihada kubwa ili kufikia malengo na matarajio ya serikali na wananchi kwa ujumla,”amesema.

Mradi wa Kisorya –Rugezi

Akizungumzai mradi wa Kisory-Rugezi wenye thamani ya Sh bilioni 5.5,  Mhandisi Kilahala amesema mkataba wa ujenzi ulisainiwa Juni 3, 2021 Mkandarasi  ambaye ni Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Boatyard alianza kazi rasmi Desemab 15, 2021 baada ya kupewa malipo ya awali na kazi inatarajiwa kukamilika Aprili 15, 2023.

Ameeleza kwamba kivuko  hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 800 kati yao 400 watakaa na 400 watasimama, tani 170 za mizigo ikijumuisha magari madogo 22,  kitafungwa  vifaa vya kisasa vya kuongozea, tahadhari na uokozi kulingana na viwango vya kimataifa  maana ujenzi wake umezingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.

“Kivuko hiki kikikamilika kitawapatia wananchi wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza uhakika wa usafiri unaowaunganisha na wilaya ya Bunda iliyopo Mkoa wa Mara na maeneo mengine jirani hivyo wataweza kukuza uchumi wao na  kupata huduma mbalimbali za kijamii bila kujali ziko wilaya ipi kati ya hizo mbili,”amesema na kuongeza.

“Temesa tunaendelea kuwaomba watumiaji wa vivuko vyoye vilivyopo  nchini tushirikiane kuvilinda  kama tunavyolinda mali zetu binafsi maana ni mali yetu sote, serikali inatumia fedha nyingi sana kuvijenga pia wateja wetu wanaovitumia walipe nauli elekezi ili tuweze kumudu gharama za uendeshaji waendelee kunufaika na huduma iwe endelevu,”amesisitiza Mhandisi Kilahala.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amesema serikali inaendelea  kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara na reli zinazounganisha nchi ya Tanzania na jirani lengo ni kurahisisha shughuli za uwekezaji na ufanyaji wa biashara za mipakani na usafirishaji wa bidhaa  zinazozalishwa nchini maana Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ambao utahitaji  fursa za masoko ya kikanda na Kimataifa.  

“Temesa mtendeeni haki Rais wetu kwa kusimamia vizuri miradi yote ambayo mnaitekeleza ili nia yake iweze kutimia  maana miradi hiyo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) ya mwaka 2020/2025.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Boatyard, Major Songoro amesema wamejipanga kufanya kazi kwa kasi na kwa weledi ili kivuko hicho kikamilike kwa wakati ambapo alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa hivyo kuwapa miradi mbalimbali ya maendeleo ili waijenge.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles