*Kimo cha Rugezi –Kisorya kinachojengwa na Kampuni ya songoro Marine Transport Ltd boatyard
Na Clara Matimo, Mwanza
Imeelezwa kwamba mwaka huu wa fedha 2022/2023 serikali itatekeleza ujenzi na ukarabati wa miradi 32 ya vivuko pamoja na miundombinu yenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 60 lengo likiwa ni kuboresha na kutatua changmoto za usafiri na usafirishaji kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamebainishwa Oktoba 18, 2022 na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme(Temesa), Mhandisi Lazaro Kilahala wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa ujenzi wa kivuko kipya cha Kisory Rugezi kinachojengwa na Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Boatyard ya mkoani Mwanza kwa gharama ya Sh bilioni 5.5.
Mhandisi Kilahala amefafanua kwamba kati ya miradi hiyo miradi saba ambayo itagharimu Sh bilioni 33.2 ni ya ujenzi wa vivuko vipya ambavyo ni Kisorya –Rugezi, Bwiro- Bukondo, Nyakarilo-Kome, Mafia–Nyamisati na Ijinga- Kahangala hadi sasa viko katika hatua mbalimbali za ujenzi maana wamekwishasaini mikataba na wakandarasi wamekwishalipwa malipo ya awali.
“Vivuko viwili ambavyo ni Buyagu-Mbalika na Magogoni –Kigamboni viko kwenye hatua za manunuzi pia mwaka huu wa fedha serikali itakarabati jumla ya vivuko 14 kwa gharama ya Sh bilioni 22.99 ambavyo ni Mv Misungwi, Kazi, Musoma, Sabasaba, Tanga, Nyerere, Magogoni, Mara, Kitunda, Kilombero II, Ruhuhu, Old Ruvuvu, Kome II na ujenzi.
“Vilevile tutafanya ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya vivuko ikiwemo madaraj ya kusimamia na majengo ya abiria ambapo tutatekeleza jumla ya miradi 11 yenye thamani ya Sh bilioni 4.1 hivyo serikali itatumia jumla ya Sh bilioni 60.3 kutekeleza ujenzi wa miradi hiyo yote ya vivuko ambayo tayari mikataba imesainiwa na kazi inaendelea,”amesema Mhandisi Kilahala na kuongeza:
“Tunaishukuru sana serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kutuwezesha kifedha kuweza kutekelza miradi hiyo ambayo lengo lake ni kutatua changamoto za wananchi nasi kama watendaji tunaahidi kufanya kazi kwa weledi na jitihada kubwa ili kufikia malengo na matarajio ya serikali na wananchi kwa ujumla,”amesema.
Mradi wa Kisorya –Rugezi
Akizungumzai mradi wa Kisory-Rugezi wenye thamani ya Sh bilioni 5.5, Mhandisi Kilahala amesema mkataba wa ujenzi ulisainiwa Juni 3, 2021 Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Boatyard alianza kazi rasmi Desemab 15, 2021 baada ya kupewa malipo ya awali na kazi inatarajiwa kukamilika Aprili 15, 2023.
Ameeleza kwamba kivuko hicho kikikamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 800 kati yao 400 watakaa na 400 watasimama, tani 170 za mizigo ikijumuisha magari madogo 22, kitafungwa vifaa vya kisasa vya kuongozea, tahadhari na uokozi kulingana na viwango vya kimataifa maana ujenzi wake umezingatia sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“Kivuko hiki kikikamilika kitawapatia wananchi wa Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza uhakika wa usafiri unaowaunganisha na wilaya ya Bunda iliyopo Mkoa wa Mara na maeneo mengine jirani hivyo wataweza kukuza uchumi wao na kupata huduma mbalimbali za kijamii bila kujali ziko wilaya ipi kati ya hizo mbili,”amesema na kuongeza.
“Temesa tunaendelea kuwaomba watumiaji wa vivuko vyoye vilivyopo nchini tushirikiane kuvilinda kama tunavyolinda mali zetu binafsi maana ni mali yetu sote, serikali inatumia fedha nyingi sana kuvijenga pia wateja wetu wanaovitumia walipe nauli elekezi ili tuweze kumudu gharama za uendeshaji waendelee kunufaika na huduma iwe endelevu,”amesisitiza Mhandisi Kilahala.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Adam Malima amesema serikali inaendelea kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara na reli zinazounganisha nchi ya Tanzania na jirani lengo ni kurahisisha shughuli za uwekezaji na ufanyaji wa biashara za mipakani na usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini maana Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kujenga uchumi wa viwanda ambao utahitaji fursa za masoko ya kikanda na Kimataifa.
“Temesa mtendeeni haki Rais wetu kwa kusimamia vizuri miradi yote ambayo mnaitekeleza ili nia yake iweze kutimia maana miradi hiyo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) ya mwaka 2020/2025.
Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Songoro Marine Transport Ltd. Boatyard, Major Songoro amesema wamejipanga kufanya kazi kwa kasi na kwa weledi ili kivuko hicho kikamilike kwa wakati ambapo alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwaamini wakandarasi wazawa hivyo kuwapa miradi mbalimbali ya maendeleo ili waijenge.