27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatumia Sh bilioni 5.9 ununuaji vifaa saidizi vya elimu

Asha Bani – Dar es Salaam

SERIKALI imetumia Sh bilioni 5.9 kununua na kusambaza vifaa maalumu vya kielimu saidizi katika shule za msingi na sekondari zinazopokea wanafunzi wenye mahitaji maalumu nchini.

Hayo yamesemwa juzi Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku 10 ya Tehama na teknolojia saidizi kwa wakufunzi na walimu wenye mahitaji maalumu, wanaofundisha shule za sekondari, ili kuwajengea uwezo wa matumizi ya teknolojia hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao.

Dk. Akwilapo alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na shime sikio kwa wanafunzi wenye baki ya usikivu, mashine za kuandikia maandishi ya breli na vivunge vyenye fimbo nyeupe kwa wasioona.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Rais Dk. John Magufuli, pia Serikali imefanya upanuzi na ukarabati wa Chuo cha Ualimu Patandi ili kuongeza udahili wa walimu kutoka 300 na kufikia 450 kwa mwaka wa masomo 2019/20.

Pia alisema Serikali imejenga shule ya sekondari ya mfano katika chuo hicho, yenye uwezo wa kudahili wanafunzi 640 wenye mahitaji maalumu.

“Shule hiyo itasaidia wanachuo kufanya mazoezi ya kufundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu kwa vitendo na kuwa mahiri katika fani wanazosomea.

“Mnaweza kuona jitihada ambazo Serikali imekuwa ikizifanya. Nitoe wito kwa familia na wadau wa maendeleo kuendelea kuona umuhimu wa kuchangia juhudi za Serikali katika kuwapatia huduma stahiki wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ujifunzaji,” alisema Dk. Akwilapo.

Aliongeza kuwa ushiriki wa jamii ni muhimu kwani masuala ya watu wenye ulemavu ni mtambuka, hivyo jitihada za pamoja zinahitajika ili kufikia malengo yaliyoainishwa katika miongozo ya kitaifa na kimataifa.

Akizungumzia mafunzo ya Tehama na teknolojia saidizi yanayotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Akwilapo alisema yanalenga kuwajengea uwezo wakufunzi na walimu wa sekondari wasioona, viziwi na wenye ualbino katika matumizi ya Tehama na teknolojia saidizi ili kuboresha ufundishaji katika vyuo vya ualimu na shule za sekondari nchini.

Alisema mafunzo hayo yatawapatia maarifa na stadi kuhusu mfumo, vipengele na utendaji kazi wa kompyuta, utumiaji wa programu saidizi za sauti na kukuza maandishi katika kompyuta, kupata stadi za matumizi ya mitandao katika kutafuta na kutuma taarifa mbalimbali katika tovuti na barua pepe pamoja  na kutumia kikamilifu maudhui ya kielektroniki katika ufundishaji na ujifunzaji.

Naye Kaimu Kamishna wa Elimu, Paulina Mkonongo,  alisema kufanyika kwa mafunzo hayo ni mkakati endelevu wa Serikali kuhakikisha elimu bora inatolewa kwa makundi yote, ikiwamo kuimarisha mafunzo kazini kwa kundi hili maalumu.

Awali Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu Maalumu, Greyson Mlanga, alisema kuwa mafunzo hayo yana jumla ya washiriki 140 wenye mahitaji maalumu, wakiwamo viziwi 37, wasioona na wenye uoni hafifu 103 kutoka vyuo vya ualimu vya Serikali na walimu wa shule za sekondari nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles