22.9 C
Dar es Salaam
Monday, September 9, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatumia bilioni 172 kulipa madeni watumishi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema katika kipindi cha Mei, 2021 hadi sasa Serikali imetumia sh. 172.614 bilioni kulipa madeni mbalimbali ya watumishi wa umma, huku ikiendelea kufanyia kazi suala hilo ili lisiendelee kuwa kero kwa wastaafu katika kumudu maisha yao.

Pia, Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) uhakikishe unatumia fedha na rasilimali za chama hicho kwa kuwahudumia wanachama wao wote bila ubadhirifu.

Waziri Mkuu ametoa kauli leo Jumatano, Agosti 25 alipofungua mkutano wa TALGWU uliofanyika katika jijini Dodoma.

“Ninawaagiza waajiri wote wazingatie kanuni za kudumu katika utumishi wa umma za mwaka 2009 ili kuondoa changamoto ya watumishi kutolipwa gharama za kurejeshwa nyumbani na stahiki zao nyingine mara baada ya kustaafu,”amesema Majaliwa.

Aidha Waziri Mkuu ametoa wito kwa TALGWU na kuwasihi waendelee kushirikiana na kuwajibika kwa kuzingatia uadilifu kwani kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ni silaha kuu katika kufikia malengo ili kupunguzia mzigo Serikali.

“Ninawahakikishia kwamba, wakati wote serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyama vya wafanyakazi katika kushughulikia maslahi kwa watumishi. Vilevile, hakikisheni fedha na rasilimali za chama zinatumika katika kuwahudumia wanachama wenu bila ubadhirifu,” amesema.

Pia ametoa rai kwa viongozi watakao fanikiwa kupita katika uchaguzi utakaofanyika leo wahakikishe wanaenda kutekeleza majukumu yao ya kikatiba kwa weledi na kwa kuweka maslahi ya wanachama wao mbele.

Amesema hadi sasa zipo halmashauri 18 ambazo hazijaunda mabaraza ya wafanyakazi, hivyo amemuelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama kuwaagiza makatibu wakuu wa wizara husika wahakikishe mabaraza hayo yanaundwa kabla ya Septemba 30, 2021.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles