27.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 5, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI YATOA UFAFANUZI WA ZIKA

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amewataka Watanzania kutokuwa na hofu kwa sababu haijathibitishwa kuwapo kwa virusi vya zika hapa nchini.

Akitoa ufafanuzi zaidi wa taarifa iliyotolewa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana iliyotolewa na NIMR juzi, alisisitiza kuwa taarifa hiyo ni matokeo ya awali ya utafiti wa ubora wa kipimo cha kupima ugonjwa wa chikungunya na zika.

Katika taarifa hiyo, Mkurugenzi wa NIMR, Dk. Mwele Malecela, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kwamba wamegundua uwapo wa virusi hivyo hapa nchini.

“Mwishoni mwa Janauri, mwaka huu wizara tulitoa tamko kwamba zika haijaingia nchini, napenda kuwatoa hofu Watanzania kwamba hadi sasa bado haijathibitika kuwa ugonjwa huo umeingia nchini.

“Napenda wananchi waelewe kwamba taarifa iliyotolewa na NIMR ni matokeo ya awali ya utafiti wa ubora wa kipimo hicho, ambapo baada ya NIMR kumaliza utafiti wao, yatapimwa tena kupitia vipimo vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Baada ya kuthibitishwa wizara inakuwa na mamlaka ya kuyatangaza matokeo hayo, kwa hiyo nataka ieleweke kwamba kuna utaratibu wa kutoa taarifa kwa magonjwa ya kuambukiza na ya hatari kama zika, ebola na mengineyo na wizara imeandaa mkakati unaoeleza juu ya ufuatiliaji wa ugonjwa huu,” alisema Ummy.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohamed Kambi, alisema Serikali inafuatilia kwa karibu matokeo hayo yaliyotolewa na NIMR.

“NIMR walichofanya ni kufanya utafiti wa kutathmini ubora wa kipimo kinachoweza kuja kutumika kupima magonjwa ya zika na mengine, kiutaratibu hizo zinakuwa ni hatua za awali baadaye matokeo yanayotokea hapo inabidi yaangaliwe zaidi na wataalamu.

“Tukubaliane vizuri kuhusu yale matokeo kama yamefuata zile taratibu zote za kitaalamu, kisayansi na baadaye ni muhimu katika kufanya utafiti wa kuangalia uwezo na ubora wa kipimo kifanyiwe ulinganifu na vipimo ambavyo tunaita gold standard ambavyo ndivyo vipimo vya uthibitisho wa kuwepo au kutokuwepo ugonjwa wa zika.

“Nasema hivyo kwa sababu hizi clips za kufanya diagnosis zinatakiwa ziwe kidogo za bei nafuu ukilinganisha na vile vipimo vya ‘gold standard’, sasa unapojaribu kufanya vipimo hivi lazima uvilinganishe na vile vya ‘gold standard’ (vya uhakika) kwamba ugonjwa upo au haupo.

“Kwa hiyo walichokifanya NIMR ni kupeana taarifa za awali kuhusu kazi waliyofanya katika mikoa ya Morogoro na Geita, matumaini yangu itafanyiwa tathmini ya kisayansi ili wanasayansi wajiridhishe kwamba imefuata taratibu zote na yale matokeo yakaendelezwa zaidi na baada ya hapo tutajiridhisha kuwapo au kutokuwapo kwa ugonjwa huu,” alisema.

Hata hivyo, alisema ugonjwa huo unapaswa pia kuripotiwa kimataifa na upo utaratibu maalumu wa kuitoa na taarifa hiyo lazima ifike wizarani, ipitiwe na hutolewa na mratibu anayepaswa kuripoti kimataifa.

Naye Dk. Malecela alisema matokeo ya awali ya utafiti huo yalionesha kuwapo kwa virusi hivyo lakini watu waliokutwa navyo hawakuonyesha dalili wala madhara yanayohusiana na zika.

“Hatukuona dalili kama ile ya kichwa kidogo, tulikuwa tunaainisha na katika uainishaji huo tuliona virusi hivyo lakini haimaanishi kuna uthibitisho.

“Nasisitiza hatuna mamlaka ya kutangaza kwamba upo, wizara ndiyo huthibitisha kulingana na utaratibu maalumu uliowekwa, NIMR tunaendelea kufanya utafiti wa zika, dengue na chikungunya na matokeo ya tafiti hizo tutayakabidhi kwa wizara pindi zitakapokamilika,” alisisitiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles