23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatoa Sh bilioni 10 kuipa nguvu Tazara

Na Mwandishi wetu-Mbeya

SERIKALI imetoa Sh bilioni 10 kufufua Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) ili kuiongeza mtaji na kufikia lengo la kujiendesha kibiashara.

Akizungumza mkoani Mbeya mara baada ya kukagua vichwa viwili vilivyokamilika baada ya kufungwa mashine mpya za kufua umeme, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema kukamilika kwa ukarabati huo kutaongeza usafirishaji wa mzigo kwa mamlaka.

“Makusudi makubwa ya Serikali kuwekeza fedha hizi ni kuhakikisha mnafanya biashara na kurejesha mzigo wa tani milioni tano mnaotakiwa kuusafirisha kwa mwaka,” alisema Kamwelwe.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ilisema fedha hizo zilizotolewa zimeshanunua mashine mpya za kufua umeme takribani 42 ambazo zitafungwa kwenye vichwa saba.

Meneja Karakana ya Tazara mkoani humo, Ezekiel Mong’ateko, alisema hadi sasa vichwa viwili vimeshakamilika na mwishoni mwa mwezi huu kichwa cha tatu kitakamilika ambapo kimoja kina uwezo wa kusafirisha tani 250,000 kwa mwaka.

 “Kukamilika kwa vichwa hivi kutaongeza mzigo tunaotakiwa kuusafirisha kwa mwaka kwani kwa sasa mzigo tunaosafirisha umepungua sana na hauzidi tani laki tatu, tunaishukuru sana Serikali kwa kuiwezesha mamlaka,” alisema Mong’ateko.

Aliongeza kuwa sambamba na ukarabati wa vichwa hivyo, mamlaka inaendelea na ukarabati wa mabehewa katika karakana ya mamlaka Dar es Salaam ili kuhakikisha ukamilikaji wa vichwa hivyo unaendana na ongezeko la usafirishaji wa abiria na mizigo.

Kukamilika kwa ukarabati wa vichwa hivyo kutaongeza idadi ya vichwa 13 vilivyopo kwa sasa na kufikia 20 ambapo kila kichwa kina uwezo wa kubebatani 30,000.

Utoaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa makubaliano ya nchi mbili – Tanzania na Zambia, ambazo kwa pamoja zilikubaliana kutoa Sh bilioni 20.

Kila nchi ilitakiwa kuchangia Sh bilioni 10 ili kuifufua upya mamlaka hiyo na kuiwezesha kujitegemea mara baada ya kushuka kwa usafirishaji kutokana na upungufu wa vichwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles