27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 7, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali yatoa kauli tahadhari shambulio Dar

NORA DAMIAN Na LEONARD MANG’OA-DAR ES SALAAM

KUFUATIA tahadhari ya tishio la shambulizi la kigaidi jijini Dar es Salaam, lililotolewa na Ubalozi wa Marekani nchini, viongozi wa Serikali na polisi wamewaondoa wananchi wasiwasi huku wakisema wanaendelea kufuatilia taarifa hizo.

Juzi Ubalozi wa Marekani nchini, ulichapisha katika mtandao wake tahadhari ya shambulizi, ukisema umepata tetesi kuwa limepangwa kufanyika Dar es Salaam maeneo ya Masaki.

Tahadhari hiyo ilisema maeneo yanayolengwa ni mahoteli na migahawa ambayo hutembelewa na watalii, ikiwemo eneo maarufu la maduka ya Slipway.

Baada ya tahadhari hiyo, jana ubalozi wa nchi hiyo nchini Uganda, ulitoa tahadhari ya shambulizi nchini humo na kuwataka wananchi kuwa makini katika maeneo wanayozuru.

Hata hivyo ubalozi huo kwa tahadhari hiyo waliyotoa ya shambulizi la Dar na Uganda, ulisema; “Ubalozi hauna ushahidi wa moja kwa moja wa tishio hilo ama taarifa za muda gani mashambulizi yatatokea, hata hivyo unawaonya wananchi kuchukua tahadhari.”

TAARIFA YA KANGI LUGOLA

Kutokana na tahadhari hiyo, jana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, alisema vyombo vya ulinzi vinaendelea na uchunguzi juu ya suala hilo.

“Nataka niwathibitishie Watanzania nchi imeendelea kuwa na amani na usalama na tutahakikisha maisha na mali za wananchi zinalindwa.

“Vyombo vya ulinzi na usalama viko imara, havitikisiki, vimejipanga vizuri kwa jambo au tishio lolote la kiusalama ambalo linaweza kutokea,” alisema Lugola.

Alisema tahadhari hiyo ya kiusalama ni ya kawaida, ambayo Watanzania hawapaswi kuwa na wasiwasi kwani Serikali iko imara.

“Ni tahadhari za kawaida ambazo huwa zinatokea kama ambavyo huwa tunatoa tahadhari za mambo ya tsunami, mvua nyingi na nyingine mbalimbali.

“Kama wenzetu wameweza kuzipata na tumewasiliana nao kupitia Jeshi la Polisi, niwahakikishie Watanzania wasiwe na hofu wala wasiwasi, nchi yao iko imara, ina usalama wa hali ya juu.

“Vyombo vinaendelea kufanya kazi yake na tuviache viendelee kufanya kazi. Watanzania waendelee na shughuli zao kama kawaida, na kama taarifa hizi zipo, ni za kweli, sisi tupo imara, tunaendelea, kwahiyo hakuna sababu ya Watanzania kuwa na hofu,” alisema.

IGP SIRRO

Juzi pia Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, alikaririwa na vyombo vya habari akisema walishapata fununu za shambulio hilo kabla Ubalozi wa Marekani haujatoa tahadhari juu ya tukio hilo.

Kwa mujibu wa IGP Sirro, walipata taarifa kuhusiana na tishio hilo tangu Jumanne wiki hii na kwamba timu zao za operesheni na intelijensia zinaifanyia kazi.

Alisema taarifa hiyo inaweza kuwa ya kweli au uongo, lakini wao kama vyombo vya ulinzi huwa hawapuuzi jambo.

RC DAR

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema jiji lipo shwari na vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya kazi kama kawaida.

“Hakuna taarifa yoyote iliyotoka katika ofisi yangu wala mamlaka ya kitaifa kwa maana ya Mheshimiwa Rais. Niwatoe hofu walio kwenye mahoteli na wageni kwenye jiji letu kwamba hakuna tishio,” alisema.  

Makonda pia aliulaumu Ubalozi wa Marekani na kuutaka kuzingatia katiba na sheria za Tanzania, kwani kuna vyombo maalumu vya kutangaza kama kuna hali ya hatari.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiswaji Jamii, Kamishna wa Polisi Musa Ali Musa, alisema wameyasikia matishio hayo kutoka katika vyanzo vilivyoyatoa na kwamba kazi yao ni kuhakikisha nchi haina matishio ya aina yoyote.

“Nchi bado ni shwari, hatujaweza kuona matukio makubwa kama yanavyoelezwa, inawezekana yapo, lakini sisi tunaendelea kuyafanyia kazi ili kuhakikisha tunabaki katika mazingira salama.

“Niwahakikishie wananchi kuwa Jeshi la Polisi lipo na linaendelea na mikakati yake, na moja ya mikakati yake ni kuona kwamba linawashirikisha wananchi na makundi mbalimbali ya watu.

“Kama tishio hili utaona linahusu sehemu kubwa ya hoteli, lakini tutashirikisha makundi ya watu ili kuona tunabaki salama ili nchi iendelee kuwa salama,” alisema Kamishna Musa.

MAENEO YALIYOTAJWA

Kutokana na tishio hilo, MTANZANIA lilitembelea maeneo yaliyotajwa kukabiliwa na tishio hilo la kigaidi, ikiwamo hoteli mbalimbali za kitalii na kukuta shughuli zikiendelea kama kawaida.

Gazeti hili lilishuhudia wageni kutoka maeneo mbalimbali wakiingia katika Hoteli ya Coral Beach maarufu kama Best Western iliyopo Masaki.

Mmoja wa wafanyakazi wa hoteli hiyo, Ibrahim Kasu, ambaye hakutaka kulizungumzia suala hilo kwa undani kwa kuwa si msemaji wa hoteli hiyo, alisema kwao suala la ulinzi wamekuwa wakilipa uzito mkubwa hata kabla ya kuwapo kwa tishio hilo.

“Siku zote tunahakikisha tunao askari wa kutosha kufanya ukaguzi, kila mgeni anayeingia ni lazima kujua anakwenda wapi na anakwenda kufanya nini,” alisema Kasu.

UBALOZI WA MAREKANIWAKIRI KUFANYA MAKOSA

Katika hatua nyingine Serikali imemwita Kaimu Balozi wa Marekani kutoa ufafanuzi wa taarifa yao ya kuwapo tishio la usalama nchini.

Taatifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kitengo cha Mawasoliano cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dar es Salaam jana, ilisema katika kikao hicho Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Faraji Mnyepe alikutana na kufanya mazungumzo ya kina na mwakilishiwa balozi wa Marekani, Ann Marie Warmenhoven.

“Ubalozi umetambua na kukiri ujumbe umetumwa na wao, lakini tumewatka wafuate taratibu za kidiplomasia,”ilisema taarifa hiyo.

Ilisema Ubalozi wa Marekani umekiri umefabnya makosa ya kutoa tetesi ambazo hazikulenga raia wa Marekani pekee, bali raia wote wakitambua hawana mamlaka ya kufanya hivyo.

Taarifa hiyo ilisem aujumbe huo umezua taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, wizara hiyo imeukmbusha Ubalozi wa Marekani ukuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani mote katika utoaji wa taatrifa za aina hii.

Mnyepe amewataka wananchi na jumuiya za kimataifa na wageni mbalimbali waliopo nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

“Mpaka sasa hakuna tarifa yoyote iliyothibitishwa ya kuwapo tishio la aina hii nchini, vyombo vya ulinzi na usalama vimejizatiti kukabiliana na tishio lolote,”ilisema taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles