26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

SERIKALI YATISHIA KUIFUTA LINO AGENCY YA LUNDENGA

Na MAREGESI PAUL-DODOMA

SERIKALI imesema inaweza kuifuta Kampuni ya Lino Agency chini ya Mkurugenzi wake, Hashim Lundenga, inayoandaa shindano la urembo la Miss Tanzania, kama kampuni hiyo haitatoa zawadi kwa mshindi wa shindano hilo kwa mwaka 2016/17, Diana Edward.

Taarifa hiyo ilitolewa bungeni juzi na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura, alipokuwa akihitimisha mjadala wa hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18 iliyokuwa imewasilishwa na Waziri wa Wizara hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Pamoja na tishio hilo, Wambura aliitaka kampuni hiyo ikabidhi zawadi hiyo ya gari kwa mshindi kabla hatua zaidi hazijachukuliwa.

"Kampuni hiyo inapaswa kutoa zawadi kwa mrembo huyo kufikia Juni mwaka huu, vinginevyo tutalazimika kuchukua hatua zaidi.

"Kama itashindwa kutii agizo hilo, basi tutalazimika kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na kuiondoa katika uandaaji wa shindano hilo," alisema Wambura.

Pamoja na kuzungumzia zawadi hiyo, naibu waziri huyo alizungumzia washindi wengine wa shindano hilo na kusema nao walitakiwa kupewa zawadi zao kwa mujibu wa taratibu zilizokuwa zimewekwa.

“Pamoja na kwamba mshindi wa kwanza hakupata zawadi yake, wale washindi wengine nao walitakiwa kupewa zawadi zao walizostahili.

"Kwa kuwa lengo letu ni kuhakikisha shindano hilo linafanyika vizuri, Serikali imefanya marekebisho ya kasoro ambazo zimekuwa zikitokea katika mashindano ya urembo likiwamo hilo la Miss Tanzania.

Wakati huo huo, Naibu Waziri huyo aliliambia Bunge, kwamba Serikali itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wanaokiuka taratibu na sheria za mashindano bila sababu za msingi.
 

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles