MBUNGE wa Ole, Rajab Mbarouk Mohamed (CUF), ameitaka Serikali kukiri kushindwa kutekeleza ahadi za Rais Jakaya Kikwete kwa kuwa muda wa utekelezaji wake umekwisha.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, alisema kitendo cha Serikali kushindwa kukamilisha ahadi ya Kikwete ya kujenga barabara ya kilomita 2.5 ya Singano kwa Mkocho hadi Kivinje ni dalili ya kushindwa kwa Serikali hiyo.
“Kwanini Serikali hii ya CCM sasa isiwathibitishie wananchi kwamba imeshindwa kutekeleza ahadi hii, kwa hiyo imewakosea wananchi hivyo wawanyime kura katika Uchaguzi Mkuu,” alihoji Mbarouk.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Kassim Majaliwa, alisema ahadi hiyo itakamilishwa kwa wakati.
“Sasa badala ya kujenga kilomita 2.5, sisi tutajenga kilomita 4.5, hii inadhihirisha jinsi Serikali ilivyo imara hivyo wananchi waendelee kuiamini,” alisema Majaliwa.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara (CUF), Majaliwa, alisema halmashauri imeshaifanyia usanifu barabara hiyo na imejulikana kwamba zinahitajika Sh bilioni 1.487 kwa ajili ya kujenga kilomita 4.5.
“Katika mwaka wa fedha wa 2013/2014, halmashauri ilipelekewa shilingi milioni 450 kuanza ujenzi.
“Katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 zilitolewa shilingi milioni 500 ili kuendeleza ujenzi wa barabara hiyo na kazi inayoendelea ni uwekaji wa changarawe,” alisema Majaliwa.
Alisema katika mwaka wa fedha wa 2015/2016, Serikali itatoa Sh milioni 650 ili kukamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Katika swali lake, Bungara alitaka kujua kauli ya Serikali kuhusu ahadi ya Kikwete.