29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yatakiwa kufuata mipango miji

Bonaventura BayaNa Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BARAZA la Taifa la Mazingira (NEMC) limeitaka Serikali kuhakikisha inatekeleza ramani za mipango miji kama zilivyo kuepuka uharibifu wa mazingira unaotokana na ujenzi holela.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bonaventura Baya, aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipotoa taarifa ya jinsi    Serikali isivyofanya vizuri katika suala la mipango miji.

Baya pia alizungumzia kukosekana mipango ya pamoja ya vyombo vinavyoshughulikia masuala ya ardhi.

“Kama Serikali hatujafanya vizuri kwenye suala la mipango miji kutokana na vyombo vyake kufanya kazi kila kimoja kivyake bila kuwapo mipango ya pamoja, hususan inayohusu utoaji wa vibali mbalimbali.

“Kutokana na ukuaji wa kasi wa miji kama vile Dar es Salaam ambao ni wa nne duniani kwa miji inayokua kwa kasi, ni lazima Serikali ihakikishe inatekeleza ‘master plan’ kama zilivyo kuepuka ujenzi na shughuli nyingine kufanyika  holela,” alisema.

Alisema ongezeko la watu Dar es Salaam ndiyo changamoto kubwa katika mipango miji.

“Hali hiyo imesababisha uhaba wa viwanja vilivyopimwa jambo ambalo limesababisha watu kujenga holela katika maeneo yasiyoruhusiwa kwa makazi,” alisema.

Alisema changamoto nyingine ni uhaba wa miundombinu ya huduma za jamii kama vile huduma za maji taka, sehemu za kutupia taka pamoja na uwezo mdogo wa taasisi kutoa huduma kutokana na uhaba wa rasilimali watu, fedha na teknolojia.

Akizungumzia kusimamishwa kwa bomoabomoa, alisema Serikali ilichukua uamuzi huo kukamilisha mipango ambayo inaonekana isipokamilika kutakuwa na athari nyingi.

“Hatua ya bomoabomoa imepata changamoto nyingi yakiwamo malalamiko zaidi ya 500 ya watu ambao walidai wana leseni za makazi, vibali na wengine kwenda mahakamani kupinga hatua hiyo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles