31.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 5, 2022

Contact us: [email protected]

Serikali yataja kinachowaponza wenye mahoteli Dar

gaudence-milanziNA KOKU DAVID, DAR ES SALAAM

PAMOJA na kuporomoka kwa biashara ya hoteli katika kipindi cha hivi karibuni, serikali imewataka wamiliki wa vitegauchumi hivyo kuwa wabunifu kwa kuwekeza nje ya miji ya Dar es Salaam na Arusha ili kutumia fursa mbalimbali kwa ajili ya soko la utalii na hoteli barani Afrika.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, katika mkutano mkuu wa awamu ya nne wa hoteli za Afrika, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi, alisema njia za kuingiza pesa katika hoteli ni nyingi na kwamba kinachotakiwa ni ubunifu pamoja na kuitisha mikutano mbalimbali, ikiwemo ya kimataifa, ambayo itawezesha kuingiza kipato.

Alisema Tanzania kuna hoteli takribani 385 zenye hadhi ya kupokea watalii, lakini changamoto iliyopo ni kwamba hoteli nyingi zipo katika jiji la Arusha na Dar es Salaam, ambayo ina hoteli 291.

Alisema katika mkutano huo, miongoni mwa majadiliano yaliyofanyika ni kuwaomba wawekezaji kutumia fursa hiyo kuwekeza kwa kujenga hoteli katika maeneo mbalimbali ya mikoa mingine.

“Kwa mfano kama kule Mkoa wa Lindi na Mtwara ambako kuna ugunduzi wa gesi wawekezaji wanaweza kujenga mahoteli kule badala ya kutegemea hizi zilizopo Dar es Salaam,” alisema Milanzi.

Alisema utalii unaliingizia Taifa mapato kwa asilimia 17 na kwamba kama utaendelezwa vizuri mapato yataongezeka zaidi ya hapo na kuweza kufikia lengo la serikali la kuifanya kuwa ya viwanda.

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Utalii Tanzania, Richard Rugimbana, alisema mkutano huo unalenga kulinganisha maendeleo ya hoteli katika nchi za Afrika, ikiwa ni pamoja na kupata taarifa za maendeleo yake na changamoto inazozikabili.

Alisema taarifa iliyotolewa katika mkutano huo inasema dunia nzima, Afrika inapata watalii asilimia 5 na ile asilimia 95 wanakwenda Marekani, bara la Ulaya na bara la Asia.

Alisema utalii wa Tanzania unakuwa na changamoto kutokana na kutokuwa na matangazo ya kutosha, ikiwa ni pamoja na miundombinu mibovu.

Lieve Noppen, ambaye ni Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya LNoppen Group, alisema wamefanya mkutano huo nchini kutokana na fursa zilizopo, hasa katika ukarimu na utalii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,586FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles