22 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Serikali yasitisha ujenzi wa stendi mpya Arusha

JANETH MUSHI – ARUSHA

SAKATA la ujenzi wa Stendi Kuu ya Mabasi ya Jiji la Arusha, limechukua sura mpya baada ya serikali mkoani hapa kusitisha mchakato wa ujenzi huo hadi pale masuala yanayoleta sintofahamu yatakapofanyiwa kazi.

Agizo hilo limetolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, akizungumzia suala hilo  katika kikao cha Kamati ya Ushauri Mkoa wa Arusha (RCC).

Wakati uongozi wa mkoa ukitoa maagizo hayo, wiki hii Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dk.Maulid Madeni, aliwasimamisha kazi Mkuu wa Idara ya Mipango Miji na Ardhi, Dickley Nyato na Mchumi wa Jiji,Anna Mwambene, ili kupisha uchunguzi wa eneo la ujenzi Stendi ya mabasi  eneo la Oloresho, Kata ya Olasiti.

Dk. Madeni alisema ilibainika kuwepo kwa ubadhirifu huo  wa zaidi ya Sh bilioni 1.9 za ununuzi wa eneo hilo  la ekari 29.9  na kulipa fidia kwa wakazi waliokuwepo ili kupisha ujenzi wa kituo hicho kikubwa cha mabasi.

Akizungumza katika RCC, Gambo alisema ameona ni muhimu kulitolea ufafanuzi hasa akiwa kama Msemaji Mkuu wa Serikali katika ngazi ya mkoa, kutokana na suala hilo kusemwa na kusambaa katika mitandao mingi.

“Nilidhani nitoe maelezo haya ila  kwa ujumla wake na kuanzia sasa hivi ya ujenzi wa stendi ya mkoa, umesimamishwa mpaka masuala yote ya msingi ambayo yanaleta sintofahamu yatakapofanyiwa kazi na serikali itakapotoa maelekezo mengine,” alisema Gambo

Akizungumzia mchakato huo alisema wakati mchakato wa maamuzi ya ujenzi wa stendi hiyo yamefanywa na halmashauri katika ngazi ya Baraza la Madiwani na kwenye vikao  mwaka 2011/12 , lilipendekeza kujenga stendi kwenye maeneo mawili ya Moshono na Olasiti na jiji lilipoingia katika Master Plan (Mipango Miji), waliamua kuchagua eneo moja.

“Jiji walikubaliana wajenge eneo moja la Olasiti na na kuliacha eneo la Moshono kwa madai kuwa baadhi ya maeneo ya Moshono yako Halmashauri ya Wilaya ya Arusha DC, wakaamua kuchagua Olasiti,” alisema

Alisema kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa, viongozi wa wilaya na halmashauri walikwenda kuangalia eneo hilo la Olasiti na kuwa katika mchakato wote kuna tathmini ya awali ilikuwa imefanyika ya mchakato wa fidia kwa upande wa Moshono na Olasiti ambapo taarifa inaonyesha gharama yake ilikuwa zaidi ya Sh bilioni 2.6

“Kama mnavyofahamu taratibu zilivyo za kufanya uthamini, ukishafanya uthamini ikipita miezi sita kama haujalipa watu uliowafanyia uthamini lazima kuna calculation zinatakiwa zipigwe kuna interest inawekwa unatakiwa ulipe,ndipo mchakato uweze kuendelea.

“Wakati nakwenda kutembelea eneo la Olasiti tulikuta tayari gharama za awali zimeshazungumzwa za mwaka 2011/12, lakini wakafanya tena uthamini mwingine wa makadirio na wakapata Shilingi bilioni 1.7 na baadaye wakafanya calculation nyingine ikafika Sh bilioni 1.9,” aliongeza

Gambo alisema jiji walielekezwa kufanya tathmini upya ili fedha inayotakiwa kutolewa kwa ajili ya fidia iendane na hali ya sasa ambapo baada ya muda mfupi waliwasilisha barua kuwa hawawezi kulipa fidia Olasiti, kwa sababu fidia ni kubwa ikidaiwa  kuna mafisaidi wamechukua eneo hilo.

“Jiji walidai wanadhani wakilipa fidia hiyo watakuwa wamelipa mafisadi.Wakasema wamepata eneo lingine la bure Bondeni City ambapo jiji wameingia mkataba na mmiliki wa eneo hilo ambaye ni mtu binafsi,”

KAMATI

Alisema aliunda kamati iliyowashirikisha watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama, Katibu Tawala wa Mkoa, wataalamu kutoka jiji na wilaya kwa lengo la kufuatilia maeneo hayo yote mawili ila hadi sasa kamati hiyo haijatoa majibu.

“Mpaka tunavyozungumza hiyo kazi haijakamilika na wala hata  hawajaleta taarifa ofisini kwangu, lakini naona matangazo na maneno mengi katika maeneo mengine,” alisema

Kuhusiana na hoja ya kuwa eneo la Olasiti lilinunuliwa na mafisadi ambao ndiyo wanataka kuliuzia jiji eneo hilo, alidai hoja hiyo haina mashiko na badala yake kuwataka kuendelea na hoja ya msingi ikiwemo kupitia na kulipa fidia wakazi waliokuwa katika eneo hilo mwaka 2011/12.

“Hoja ya kwanza inayojengwa kwamba kuna mafisadi wamenunua haina msingi wowote kwa sababu watu wenye maeneo wanajulikana toka mwaka 2011/12 na orodha yake halmashauri wanayo.

 “Licha ya barabara ya Bypass kupita Olasiti lakini huhitaji kujenga hata hatua mbili za lami lakini ukijenga stendi kwenye eneo linalopendekezwa la Bondeni City,kwanza kuna kazi ambazo lazima zifanyike, ujenge kipande cha lami kilomita 0.9 kutoka barabara ya ByPass ilipo hadi eneo hilo na draja ili mabasi yaende kwa urahisi,”

 “Lakini bado eneo la Bondeni City yule mwenye ardhi ameweza kutoa ramani ya eneo lake na mpaka sasa hivi anadaiwa deni la Dola za Marekani 340,000 ambazo hajazilipia kwa ajili ya huo mchoro wenyewe,” alidai

Alidai kutokana na mvutano huo wamegundua jiji la Arusha waliingia makubaliano na mfanyabiashara mwenye eneo hilo na moja ya maelekezo wanataka kupeleka stendi katika eneo hilo ili kumsaidia aweze kuuza viwanja kirahisi ambapo jiji itapata asilimia 10 ya kila eneo litakalouzwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,504FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles