SERIKALI imetangaza utaratibu mpya wa utekelezaji wa mpango wake wa kubomoa nyumba zote zilizojengwa kinyume cha taratibu na sheria za nchi.
Imesema hivi sasa itajielekeza kubomoa nyumba zilizo ndani kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia bondeni na katika kingo za Bonde la Msimbazi.
Sambamba na hilo, imesema itaheshimu uamuzi wa mahakama dhidi ya mashauri ya watu walioweka pingamizi la nyumba zao kubomolewa na itawalipa fidia wale wote waliojenga kwenye maeneo hatarishi kwa kupewa vibali halali na Serikali na pia itafuatilia kesi zilizoko mahakamani ili ziishe haraka tayari kwa taratibu nyingine kuendelea.
Uamuzi huo wa Serikali umetangazwa jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba, mbele ya waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya mkutano wa mawaziri watatu walioketi kufanya tathmini ya mwenendo wa kazi hiyo na kuibuka na maazimio 12 yanayoelekeza namna mpya wa utekelezaji wa ubomoaji.
Mawaziri waliofikia pamoja na Makamba kufanya tathmini hiyo ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Tamisemi, George Simbachawene na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Injinia Ramol Makani.
Aidha, tangazo la uamuzi huo mpya wa Serikali limekuja ikiwa ni siku chache baada ya Rais John Magufuli kukutana kwa nyakati tofauti na marais wawili wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete pamoja na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Makamba alisema kazi ya kuwaondoa wananchi wanaoishi katika Bonde la Msimbazi itaendelea kwa utaratibu ambao hautawasababishia mateso na usumbufu.
Alisema utekelezaji wa kazi ya ubomoaji ndani ya bonde hilo utalenga makazi yote yaliyojengwa ndani kabisa ya bonde, kwenye miteremko ya kuingia bondeni na katika kingo za bonde.
Waziri Makamba alisema watu wenye nyaraka halali zilizowaruhusu kujenga walizopewa na mamlaka za umma hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga na kwamba watumishi wa umma waliotoa maeneo hayo watachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.
Akizungumzia maeneo yaliyokwishabomolewa alisema katika muda wa siku tatu kuanzia jana, kazi ya kuzoa vifusi na kusafisha maeneo yaliyobomolewa itaanza.
Akizungumzia ukiukwaji wa taratibu dhidi ya baadhi ya maofisa wa Serikali, Waziri Makamba alisema Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake wanaoendesha kazi ya kubomoa na kuweka alama ya X katika nyumba zinazopaswa kubomolewa kinyume na misingi ya sheria zinazotekelezwa.
“Serikali itawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wake ambao watakwenda kinyume na misingi ya haki na uwazi, ikiwamo wanaoweka alama za X zaidi ya mita zilizowekwa kisheria, limeanzishwa dawati la malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupokea malalamiko au maswali kuhusu kazi hii.
“Pia nyumba na majengo yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa kwa sheria zinazotekelezwa sasa hayatabomolewa isipokuwa tu pale maisha ya watu yalipo hatarini,” alisema Makamba.
Waziri huyo alizungumzia pia bomoa bomoa ya hoteli zilizobainika kujengwa katika maeneo yasiyoruhusiwa kwa kueleza kuwa Serikali haina dhamira ya kuzibomoa hoteli kubwa zilizojengwa siku nyingi karibu na fukwe za eneo la Masaki, lakini wamiliki wake watapewa masharti na miongozo ya kuhifadhi mazingira kwa mujibu wa sheria.
“Serikali haina dhamira ya kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi yao bila sababu za msingi. Lakini pia Serikali haiwezi kuruhusu wananchi waendelee kukaa katika maeneo ambayo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yanakuwa hatarini.
“Katika mafuriko ya mwaka 2011, wananchi 49 waishio mabondeni walipoteza maisha na Kurugenzi ya Hali ya Hewa imetoa taarifa ya kuwepo kwa mvua kubwa hivi karibuni kuliko zilizowahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni,” alisema Waziri Makamba.
Alirejea kukumbusha kuwa bonde la Msimbazi lilitangazwa kuwa ni eneo hatarishi kuishi binadamu tangu mwaka 1949 na baadaye 1979 na kwamba kazi ya kuwaondoa wananchi kwenye maeneo hatarishi kwa kuishi inalenga kupanua uwezo wa mito ya Dar es Salaam ili kupitisha maji ya mvua kwa kasi itayaoondoa uwezekano wa kutokea mafuriko na maafa wakati wa mvua, kuzuia milipuko ya magonjwa hasa ya kipindupindu pamoja na kuzuia uhalifu.
Sakata la Mchungaji Rwakatare
Akizungumzia sakata la nyumba ya Mchungaji Getrude Rwakatare ambaye ana zuio la mahakama na kuvunjwa kwa nyumba yake aliyojenga eneo lililo na njia ya kupitishia maji ambalo amelijaza kifusi, alisema tangu ujenzi unaanza alipigwa marufuku na mamlaka za Serikali za Mitaa lakini zilizidiwa nguvu.
“Pale Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa nyumba hiyo, lilishtakiwa mahakamani. Wakati kesi inataka kuanza kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa baraza bila kuagizwa wala kuwataarifu wakubwa zake aliingia makubaliano na mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya baraza akaondoa kesi hiyo mahakamani na kukubali kwa niaba ya baraza kutombughudhi.
“Makubaliano hayo yalisajiliwa na Mahakama kama hukumu Mei 13, 2015. Mwanasheria huyo alificha makubaliano hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba 2015 yalipogundulika na mtumishi mwingine wa baraza.
“Mwanasheria huyo alifukuzwa kazi Januari 6 mwaka huu na taarifa zake zimekwishafikishwa Takukuru. Vile vile, Ofisi ya Makamu wa Rais, imeagiza baraza kufungua shauri mahakamani la kuomba makubaliano kati yake na Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni kwa sababu yalipatikana kwa njia ya udanganyifu,” alisema Makamba.
Nyumba 18,000 zatiwa alama ya X
Wakati huo huo, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na Halmashauri za Manispaa ya Jiji Dar es Salaam, jana walitia alama ya X katika nyumba 1934.
Idadi hiyo inafikisha idadi ya nyumba 18,000 zilitiwa alama hiyo zitakazobomolewa.
Habari hii imeandikwa na Ruth Mnkeni, Tunu Nassor na Johanes Respichuis.