27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yashauriwa kuwaandaa wasomi kujiajiri

MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

MSOMI na mfanyabiashara maarufu Dar es Salaam, Tumaini Madinda, ameishauri Serikali kubuni njia mbadala itakayosaidia kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa wasomi wengi wanaomaliza masomo yao hapa nchini.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita alipozungumza na gazeti hili kwa nia ya kuisaidia Serikali kupata ufumbuzi wa tatizo hilo ambalo zaidi linawakumba vijana na kuongezeka kila kukicha. 

Madinda aliyezaliwa mkoani Dodoma miaka arobaini iliyopita, alifafanua kuwa zinahitajika juhudi za makusudi kwa Serikali, hasa wizara ya elimu kuhakikisha inaweka mikakati ya kimitaala ili kuzalisha wahitimu wanaoweza kujiajiri.

“Mimi nimehitimu shahada ya juu (Masters) ya masuala ya uwekezaji na fedha pale Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), nikaajiriwa sehemu mbili tatu kabla ya kutafakari njia mbadala iliyoniwezesha kujiajiri,” alisema Madinda.

Aidha, alisema kutokana na uongozi madhubuti wa Rais John Magufuli, anaamini Wizara ya Elimu inaweza kuwatumia wataalamu wa ndani na hata wa nje kuanzisha mfumo huo anaouona kama mwarobaini wa tatizo hilo.

“Ombi langu kwa Serikali kupitia wizara yenye dhamana ya elimu ni kwamba, wabuni njia mwafaka ziatakazozaa matunda kwa vijana na hasa watoto wetu ambao watakapofikia ngazi ya elimu ya juu watoke na ujuzi na maarifa yatakayowasaidia kujiajiri,” alisema Madinda.

Aliongeza kuwa: “Nikipata nafasi ya kuzungumza na vijana waliohitimu vyuoni na wanaoendelea na masomo, nitawashauri kukazania maarifa huku wakizingatia kuwa ajira zao zitatokana na wao wenyewe, kinyume na wengi wanaotegemea Serikali au taasisi binafsi kuwaajiri.”

Akizungumzia maisha yake kwa sasa, Madinda alisema anajishughulisha na biashara mbalimbali huku akimiliki kampuni za ulinzi na forodha akiwa ameajiri Watanzania wengi. Kama haitoshi, anamiliki mashamba makubwa mikoa ya Pwani na Dodoma na utoaji wa ushauri.

 “Kama vijana wa Tanzania tutaendelea kuiendekeza kasumba ya ‘utegemezi’ wa kuajiriwa, tutazidi kuchelewa. Lazima tuamke sasa, dunia inakwenda kasi sana, hatuna budi kuchangamka. Sayansi na teknolojia imetamalaki kila mahali, tuongeze juhudi na kutumia maarifa kuyafumbata maendeleo,” alisema Madinda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles