Serikali yashauriwa iweke utaratibu upimaji selimundu

0
740

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM 

DAKTARI Bingwa wa Magonjwa ya Watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Christina Kindole, ameishauri Serikali kuweka utaratibu wa watoto kupima selimundu baada ya kuzaliwa ili waweze kupatiwa matibabu ya haraka.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu juzi, Dk. Kindole alisema idadi ya watoto walio na ugonjwa huo inaendelea kuongezeka ambapo kliniki moja kwa wiki katika hospitali hiyo daktari huwaona watoto zaidi ya 50. 

“Hapa wagonjwa wengi wa damu tunaowaona ni wale wa sicklecell (selimundu). Kwa upande wa watoto, tunafanya kliniki kwa wiki mara moja katika kliniki hiyo wagonjwa wanaweza kuwa 30 hadi 60, inategemea kuna siku 30, 40, 50 mara nyingi mwisho 60. Sasa hivi hatuna ahadi kurudi ya mwezi mmoja au miwili, utakuta zimeshajaa, hapa ni kuanzia miezi mitatu na kuendelea.

“Kwa wenzetu wanapata watoto mapema kutokana na watoto kupimwa vipimo vyote baada tu ya kuzaliwa ikiwemo sickle cell. Sisi tunasubiria mpaka anaanza dalili za sickle cell au labda mama ana mtoto mwingine wa sickle cell unamwambia ukijifungua tena mtoto mwingine uwahi au akifikisha miezi sita.

“Nashauri Serikali kuweka mfumo wa kupima sickle cell baada ya mtoto  kuzaliwa ili watoto hao waweze kugundulika na kuanza matibabu haraka,” alisema Dk. Kindole.

Alibainisha kuwa ongezeko la wagonjwa linaweza kusababishwa na watu kupata uelewa zaidi kuhusu ugonjwa huo. 

“Wapo wanaokuja hospitali kwa ajili ya kupima, siwezi kusema tatizo linaongezeka, labda huko mwanzoni hatukuweza kuwafikia wengi kupata elimu, lakini hata sasa bado kuna wengine hawajaweza kufikiwa. 

“Hali ziko tofauti, sasa hivi kuna watu wanakuja kupima baada ya kuona dalili kwa watoto, mwingine anakuja kwa sababu ndugu yake ana selimundu anaamua kupima, na wengine wanakuja tayari wameshapata madhara yake kama kupooza au kuongezewa sana damu,” alisema. 

Hata hivyo aliwataka watu kuondokana na imani potofu ya kuwa ugonjwa huo unasababishwa na mzazi mmoja. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here