23.7 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali yapunguza tozo za mafuta

Na Ramadhan Hassan,Dodoma

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imefanya marekebisho ya tozo mbalimbali ikiwamo matumizi ya miundombinu  ya bandari,Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA),Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA),pamoja na kupunguza gharama za kuweka vinasaba kwenye mafuta kutoka sh 14 kwa lita hadi shilingi saba.

Marekebisho hayo yatawanufaisha Watanzania kwa kupunguza matumizi ya fedha kwenye manunuzi ya mafuta kwa bilioni 102 na EWURA kutaja bei mpya za mafuta.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuelekeza kupunguzwa kwa tozo  zinazotozwa na taasisi mbalimbali katika bidhaa za mafuta  hapa nchini  kwa mwaka kwa lengo la kupunguza bei ya mafuta na kuhakikisha wafanyabiashara wa mafuta wanafanya biashara katika mazingira mazuri.

Rais Samia ametoa maagizo hayo wakati akipokea  taarifa kutoka kwa Waziri wa Nishati, Januari Makamba kuhusu utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa wizara hiyo  kupitia mwenendo wa biashara ya mafuta na bei zake hapa nchini.

Akiuzungumza na Waandishi wa Habari jana Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa (EWURA) Godfrey  Chibulunje amesema Serikali imebadilisha tozo ya matumizi ya miundombinu ya bandari ambayo inatozwa kwa Dola za Marekani (USD 10MT +VAT) kwa tani na sasa itatozwa kwa shilingi ya Tanzania.

“Na pia tozo hiyo itapunguzwa kufika shilingi 15 kwa lita kutoka wastani wa shilingi 22 kwa lita na kuondoa VAT  katika tozo hii,mabadiliko haya yataleta  kwa watumiaji  mafuta kwa wastani wa shilingi bilioni 23.15 kwa mwaka  kutokana na matumizi  ya lita bilioni 3.42 kwa takwimu za mwaka 2020,”amesema.

Vilevile,amesema Serikali imepunguza tozo ya TRA ya kuchakata nyaraka  kutoka shilingi 4.8 kwa lita  na kuwa kiwango maalum  cha shilingi milioni 20 kwa kila meli ambapo kwa wastani meli saba huleta shehena ya mafuta kila mwezi.

“Pia,Serikali imepunguza tozo ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kwa shilingi moja kwa lita  na kuwa tozo ya kiwango maalum ambacho ni shilingi milioni saba kwa kila meli baada ya kutozwa kwa kila lita.

“Serikali imepunguza tozo ya TBS ya kupima ubora wa mafuta yanayoingizwa nchini kutoka shilingi shilingi milioni 1.24 kwa lita na kutozwa kwa kiwango maalum ambacho ni shilingi milioni 12.8,”amesema.

“Pia,amesema Serikali imepunguza gharama za kuweka vinasaba kwenye mafuta kutoka shilingi 14 kwa lita hadi shilingi 7 kwa lita.

“Serikali imefuta tozo ya huduma(Service Levy ) inayotozwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa  kwa Halmashauri za Temeke na Kigamboni kwa Dar es salaam  na Tanga na Mtwara  kwa wafanyabiashara wa jumla  ambao wana maghala ya kuhifadhia  mafuta ya jumla,”amesema.

Katika hatua nyingine,Kaimu Mkurugenzi huyo ametaja  bei mpya za mafuta ya Petroli,Dizeli na mafuta ya taa kuanzia kuanzia leo Oktoba 6,2021.

Amesema Dar es salaam petroli itauzwa sh 2,439, dizeli sh 2,261 na mafuta ya taa 2,188, Dodoma  petroll 2,497,dizeli 2,320 na mafuta ya taa sh 2,246.

Mikoa mingine ni Arusha, petroll sh 2,535,dizeli sh 2,301 na mafuta ya taa sh 2,272,Mwanza, petroli sh 2,469,dizeli sh 2411 na mafuta ya taa sh 2,338.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles