25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 21, 2023

Contact us: [email protected]

Serikali yapiga marufuku walimu kuingia na viboko darasani

Tiganya Vincent -Mwanza

SERIKALI imepiga marufuku walimu wanaofundisha madarasa ya kuanzia elimu ya awali hadi darasa la tatu kuingia na viboko darasani.

Kauli hiyo imetolewa juzi mjini Mwanza na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia elimu, Tixon Nzunda wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuandaa vipindi vya redio kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (MKUE-Tanzania).

Nzunda alisema kuwa vitendo hivyo vinasababisha wanafunzi wa madarasa hayo kuogopa na kutokuwa wasikivu wakati wanapofundishwa.

Kanuni ya 3(1) ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353, marejeo ya mwaka 2002, inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhabu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya viboko itolewe kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko vinne kwa tukio lolote.

Sheria inamtaka mwalimu mkuu wa shule husika kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo.

Katika hatua nyingine, Nzunda ametoa wito kwa wadau wa elimu kushirikiana na Serikali katika kujenga mazingira mazuri ya utoaji elimu nchini ikiwemo ujenzi wa madarasa, vyoo na nyumba za walimu.

Alisema hali ilivyo sasa, ili kukamilisha miundombinu na kuweka mazingira mazuri ya utaoji elimu na ujenzi wa nyumba za kuishi walimu, zinahitajika Sh trilioni 14 kutekeleza hilo katika shule za sekondari na msingi nchini kote.

Nzunda alisema Serikali peke yake haiwezi kukamilisha hilo bila kushirikiana na wadau wengine kujenga madarasa ya kutosha ili kupunguza msongamano wa wanafunzi, kuondoa uhaba wa nyumba za walimu na vyoo.

Alisema Serikali katika kukabiliana na tatizo la msongamano wa wanafunzi katika shule mbalimbali za msingi na sekondari, tayari katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita imetoa zaidi ya Sh bilioni 65 kwa ujenzi wa maboma ya madarasa 5,289 nchini kote.

Nzunda alisema kuwa fedha hizo zimesaidia kukamilisha maboma 2,392 kwa sekondari na 2,897 kwa shule za msingi nchini kote.

Alisema kuwa badala ya asasi zisizo za kiserikali (NGOs) kutumia fedha katika kutangaza changamoto na upungufu katika shule nchini kama vile msongamano na upungufu wa matundu ya vyoo, ni vema wakazitumia kushirikiana na Serikali kuboresha mazingira ya shule nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles