25.3 C
Dar es Salaam
Monday, January 30, 2023

Contact us: [email protected]

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU POMBE ZA VIROBA

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema kuanzia Machi mosi, mwaka huu Serikali itapiga marufuku matumizi ya pakiti za plastiki kufungashiwa pombe kali maarufu kama ‘viroba’.

Pia amesema wakati wowote kuanzia sasa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, atatoa tamko la Serikali kuhusu mkakati wa kudhibiti pombe hizo.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa Baraza la Taifa la Kudhibiti Dawa za Kulevya, alisema pombe zisizopimwa kihalali zinazowekwa katika viroba zinazoofisha vijana walioko shuleni na maeneo mengine.

“Dawa za kulevya zinafanana sana na vinywaji visivyopimwa, Serikali iko kwenye hatua za mwisho za kutoa tamko juu ya pombe zinazofungashwa kwenye pakiti na zisizokuwa na vipimo halisi kama gongo na nyingine,” alisema.

Juzi alipozungumza na maelfu ya wakazi wa Mji Mdogo wa Mererani wilayani Simanjiro akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Manyara, alisema tayari wamekutana na wenye viwanda na kukubaliana juu ya kuziweka katika ukubwa unaokubalika.  

“Sasa hivi viroba vimeenea kila kona hata watoto wa shule za msingi wanatumia kwa sababu ni rahisi kuweka mfukoni na kutembea navyo. Kuanzia Machi mosi tutakayemkamata ameshika pombe ya viroba sisi na yeye,” alisema.

Majaliwa alisema agizo hilo linaenda sambamba na vita dhidi ya dawa hizo kwa sababu Mererani inaongoza kwa matumizi ya dawa hizo haramu.

“Tutawakamata wanaosambaza, wanaouza na wanaokula. Hapa Mererani kuna bangi, kuna mirungi, cocaine na heroine. Mkuu wa Mkoa hapa panahitaji operesheni kupambana na dawa za kulevya. Piteni kwenye vijiwe na kukagua wale waliolegea legea kisha tuwapime,” alisisitiza.

UZINDUZI WA BARAZA

Akizindua baraza hilo linaloshirikisha wajumbe ambao ni mawaziri 10 kutoka Tanzania Bara, mawaziri watano kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), wakuu wa mikoa 12, makatibu wakuu, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na Kamishna Mkuu wa Kudhibiti na Kupambana Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, ambaye ndiye Katibu, aliwataka wakuu wa mikoa kuepuka kuwatangaza watuhumiwa wanaojihusisha na utumiaji na biashara ya dawa hizo kabla hawajafanya uchunguzi.

Majaliwa ametoa kauli hiyo baada ya hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kutaja hadharani majina ya watuhumiwa aliodai wanajihusisha na dawa za kulevya wakiwamo wasanii, wafanyabiashara na wanasiasa na kuwataka wafike Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa mahojiano.

Hata hivyo, kitendo cha Makonda kutaja majina hayo hadharani kilikosolewa na wanasheria na wabunge bungeni kwa hoja kwamba hakufuata taratibu za kisheria.

Akizungumza katika uzinduzi wa baraza hilo, Majaliwa, aliwataka wawe waadilifu na kuepuka kupokea rushwa ya kuwasamehe watumiaji au wafanyabiashara wa dawa hizo na wakithibitika watachukuliwa hatua za kisheria.

“Mmeaminiwa muwe waadilifu kwa sababu mmekabidhiwa majukumu makubwa yanayohitaji uangalifu wa hali ya juu. Sheria ya Udhibiti Dawa za Kulevya itekelezwe kikamilifu bila kumwonea mtu yeyote,” alisema.

Majaliwa alisema aliamua kuwaita wakuu wa mikoa wa majiji ambako dawa hizo huingia na kutumika kwa wingi na mikoa ya pembezoni na mipakani inayotumika kama njia za kuingizia dawa kutoka nje.

 

“Vita hii ni kubwa, inatakiwa kupiganwa kwa nguvu zote kwa sababu madhara ni makubwa kwa jamii hususani vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa. Msiogope Serikali inawategemea na itawaunga mkono katika vita mnayoendelea nayo ili tukomeshe matumizi ya dawa za kulevya nchini,” alisema.

Pia alisema biashara ya dawa hizo inashirikisha wafanyabiashara wakubwa na watu maarufu hivyo kunahitajika sauti ya pamoja kushinda vita hiyo.

Alisema Tanzania imekuwa ikitumika kama njia ya kupitisha dawa hizo kutoka nje kwenda nchi nyingine na matumizi yake pia ni makubwa hapa nchini kwa sababu kilimo cha bangi na mirungi bado ni tatizo kubwa.

Alisema katika kipindi cha Januari hadi Desemba, mwaka jana, kilo 77 za heroin zilikamatwa zikihusisha kesi 703 na kilo 32.3 za cocaine zikihusisha kesi 259.

Pia alisema kilo 78,656 za bangi zilikamatwa zikihusisha kesi 14,323 na ekari 71 za mashamba ya bangi ziliteketezwa. Alisema katika kipindi hicho pia kilo 31,463.615 za mirungi zilikamatwa zikihusisha kesi 2,362.

Alisema hadi sasa watumiaji zaidi ya 2,223 wanapata huduma za matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), hospitali ya Mwananyamala na Temeke.

Aliendelea kusema kuwa kuna huduma za upataji nafuu (sober houses) 11 kwa Tanzania Bara ambazo zimehudumia waathirika 2,325 na kwa upande wa Zanzibar kuna nyumba 12 ambazo zimehudumia waathirika 7,953.

Pia alisema vifaa vya utambuzi wa awali wa dawa za kulevya vimetolewa katika mipaka ya Tunduma, Kasumulu, Namanga, Horohoro na Mtukula na vitaendelea kukwekwa katika mipaka yote nchini.

Kuhusu kesi za dawa za kulevya, alisema kesi mbalimbali zilitolewa hukumu mwaka 2011 ambapo washtakiwa walifungwa kati ya miaka 20 hadi 30 na kutakiwa kulipa faini kati ya Sh bilioni tatu hadi 15.

Kesi hizo ni kesi namba 47/2011 iliyowahusu watuhumiwa Fred Chonde na wenzake waliohukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na faini ya Sh bilioni 15, kesi namba 87/2011 iliyomhusu Said Kimaro, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na faini ya mara tatu ya thamani ya dawa alizokamatwa nazo.

Kesi nyingine ni namba 53/2011 iliyowahusu watuhumiwa Chukudwi Denis na wenzake waliohukumiwa kifungo cha miaka 30 jela na kulipa faini ya Sh bilioni tatu na kesi namba 91/2011 iliyomhusu Mwiteka Mwandamele, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na faini ya mara tatu ya kiasi cha dawa zilizokamatwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles