Serikali yapiga marufuku KY Jelly

Ummy Mwalimu
Ummy Mwalimu
Ummy Mwalimu

NA HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAAM

SERIKALI imepiga marufuku matumizi na usambazaji wa vilainishi  kwa wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amesema hatua hiyo ni kwa ajili ya udhibiti wa Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Akizungumza  Dar es Salaam jana, alisema Serikali imezuia matumizi ya vilainishi hivyo kwa sababu vinachochea kuongezeka   vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi.

“Ni kweli Serikali imezuia vilainishi hivyo kwa sababu ya kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

“Katika   wanaume wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja, asilimia 23 wana maambukizi ya VVU.

“Katika nchi yetu hakuna  sheria inayoruhusu uhusiano wa jinsia moja na kuendelea kusambaza vilainishi hivyo ni kama kuhalalisha vitendo hivyo… mila na desturi zetu haziruhusu uhusiano huo,” alisema.

Alisema pamoja na nia njema na jitihada baina ya wizara na wadau katika mapambano dhidi ya Ukimwi, imebainika   baadhi ya wadau wanaotekelezeka shughuli za makundi maalum wamekuwa wakikiuka taratibu za  utendaji na kusambaza vilaninshi hivyo.

Waziri alisema kitu hicho ni kinyume na makubaliano waliyoyaingia na Wizara ya Afya.

Alisema wizara baada ya kubaini wadau ambao wamekuwa wakisambaza vilainishi hivyo, wadau hao wameahidi kukusanya vilainishi hivyo na kuviteketeza.

Wizara pia imekubali kushirikiana na wadau hao ili kuangalia kama kuna fedha ambazo zingetumika kununua vilainishi hivyo ziweze kupangiwa matumizi stahiki kulingana na vipaumbele  vya wizara, alisema.

“Nahitaji hizo fedha zinazotumika kununulia vilainishi wanipe niweze kujengea wodi za kina mama  na kununulia pamba na glovu kwa ajili ya  kina mama wanaotaka kuifungua kuliko kuzipeleka huko,”alisema.

Alisema   utafiti mbalimbali nchini umethibitisha kuwapo  kiwango cha juu cha maambukizi ya VVU na ni miongoni mwa makundi maalum yaliyo katika hatari zaidi ya maambukizi kuliko kiwango kilichopo ambacho kwa sasa ni asilimia 5.1.

Aliyataja makundi hayo kuwa ni pamoja na wanawake wanaofanya biashara za ngono, asilimia 26.

Wengine ni  watu wanaojidunga sindano za dawa za kulevya ambao ni asilimia 36 na wanaume wanaojihusisha na jinsia moja asilimia 23.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here