22.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 12, 2022

Serikali yapiga kufuli kiwanda bubu cha dhahabu

Na MWANDISHI WETU-KAHAMA

WAZIRI wa Madini, Doto Biteko,  amekifunga kiwanda bubu cha kuchenjua madini ya dhahabu kilichofunguliwa kinyemela katika Kijiji cha Bunanga. Kata ya Bugarama, Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Kiwanda hicho kinachomilikiwa na Simoni Shule, kipo katikati ya makazi ya watu hali ambayo inahatarisha maisha yao na kuharibu mazingira kutokana na kutiririsha kemikali za sumu.

Biteko alisema licha ya Serikali kuboresha sekta ya madini kwa wachimbaji na wafanyabiashara wadogo nchini, imebainika kuwa wapo ambao wamekuwa wakifanya shughuli za uchenjuaji wa madini ya dhahabu ikiwamo kuanzisha viwanda bubu kinyume na taratibu na kuikosesha mapato.

Hayo yaliyasema juzi baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika kijiji hicho na kubaini kuwapo kiwanda hicho bubu.

“Kiwanda hiki kipo hapa katika nyumba hii kwa kipindi cha zaidi ya miezi saba kikiendelea kufanya kazi bila kufuata sheria na taratibu zilizopo na kuipotezea Serikali mapato mengi, hivyo tutachukua hatua kali za kisheria kwa mmiliki wa mtambo huu ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia chafu kama hii,” alisema Biteko.

Aidha, Biteko aliwataka viongozi wa vijiji na mitaa wilayani humo kuhakikisha wanawafichua wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara haramu ya madini ambayo inafanyika katika makazi ya watu kinyume na sheria na kuikosesha Serikali mapato.

“Niwaagize viongozi wote wa ngazi zote nchi nzima kuhakikisha mnasimamia na kudhibiti vitendo vya biashara haramu ya madini, ambavyo vinaendelea kufanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema Biteko.

Wakati huo huo, Biteko aliliagiza Jeshi la Polisi kumkamata na kumuhoji Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Bunanga, Kajanja Kajanja na mke wa mwenye nyumba iliyobainika kuwa na mtambo wa kuchenjulia dhahabu kutokana na kuhusishwa nao.

Katika ziara hiyo, mifuko zaidi ya 44 ya kemikali zinazotumika kuchenjulia madini ya dhahabu (Kaboni) imekamatwa katika kiwanda hicho inayodhaniwa kuwa na madini ya dhahabu, huku mashine hiyo yenye uwezo wa kubeba kilo 500 za Kaboni ikiwa tayari imewekewa mzigo tayari kuanza kazi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Bunanga, Januari Luhamba, alisema baada ya kugundua shughuli zinazofanywa na kiwanda hicho katikati ya makazi ya watu katika eneo lake, alitoa taarifa kwa mamlaka za kisheria ikiwamo polisi lakini hakuona hatua yoyote iliyochukuliwa kwa wahusika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,526FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles