30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yapinga hukumu iliyoruhusu dhamana baadhi ya makosa ya jinai

NA KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

MAWAKILI nane wa Serikali wamewasilisha hoja 10  Mahakama ya Rufaa wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyoruhusu dhamana kwa baadhi ya makosa ya jinai na kutamka kuwa kifungu kinachozuia kinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mawakili hao ambao wanamwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hoja zao zilisikilizwa juzi mbele ya jopo la majaji watano akiwemo Jaji  Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika, Jacob Mwambegele, Mwanaisha  Kwariko na Ignas Kitusi.

Jopo la mawakili hao ni Wakili Mkuu wa Serikali, DK Clement Mashamba, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, Mawakili Wakuu wa Serikali, Alesia Mbuya, Faraja Nchimbi, Tumaini Kweka, Abubakar Mrisha na Narindwa Sekimanga waliwasilisha hoja wakiomba mahakama hiyo ya juu itengue maamuzi ya Mahakama Kuu.

Miongoni mwa hoja walizowasilisha ni kwamba  Mahakama Kuu ilikosea kisheria kutamka kuwa kifungu namba 148 (5) kinakiuka ibara ya 13 (3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Wanadai mahakama hiyo ilifanya makosa ya kisheria kutamka kuwa kifungu hicho namba 148 cha sheria ya makosa ya jinai hakithibitishwi na ibara ya 15 (1) na (2) (a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Warufani wanadai mahakama hiyo ilikosea kutamka kwamba kifungu hicho kilikiuka Katiba pamoja na kwamba mjibu rufaa alishindwa kuthibitisha madai yake bila kuacha shaka.

Jopo la mawakili hao linadai mahakama ilikosea kuamua kwamba Katiba ilikiukwa kwa kuangalia hoja zisizosanifiwa, ilikosea kupinga kifungu hicho bila kuzingatia shida zinazoweza kusababishwa katika mfumo mzima wa utawala wa haki za Jinai nchini.

Akijibu Mjibu rufani Dickson Sanga anayewakilishwa na Mawakili wa utetezi akiwemo Mpoki Mpoki na Jebra Kambole, aliomba rufaa hiyo itupiliwe mbali kwa sababu ina mapungufu na haina msingi wowote kisheria.

Alidai maombi ya mjibu rufani kupinga kifungu hicho cha sheria yakisikilizwa Mahakama Kuu na kutolewa uamuzi na msingi wa maombi hayo ni kuwa uhuru binafsi na dhana ya kutokuwa na hatia ni haki ya kikatiba iliyohakikishwa katika Katiba ibara ya 13(6)(b) pamoja na ibara ya 15(1) na (2) .

Mei 18 mwaka huu Mahakama Kuu ilitoa uamuzi kwamba kifungu cha148, kifungu kidogo cha tano cha sheria ya makosa ya jinai kinakiuka Katiba.

Sanga alifungua kesi hiyo Mei 9, 2019 katika Mahakama Kuu Tanga akipinga kukataliwa dhamana kwa baadhi ya makosa chini ya kifungu hicho ambapo baadaye kesi hiyo ilihamishiwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama Kuu iliweka wazi kuwa kifungu hicho cha 148 (5) kinakiuka ibara ya 13 (6) b na ibara ya 15 (2) a ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa mujibu wa ibara ya 30 (5) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mahakama ilitoa miezi 18 kwa Serikali kukifanyia marekebisho na kushindwa kufanya hivyo kwa wakati kutamaanisha kufutwa kwa kifungu hicho.

Pia mahakama hiyo ilisema muda huo wa miezi 18 hautahusu kifungu hicho sehemu ya i kinachohusu makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha ambayo yalishaondolewa katika orodha ya makosa yasiyo na dhamana.

Makosa yaliyozungumzwa ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa kifungu hicho cha sheria ni pamoja na mauaji, uhaini, biashara ya dawa za kulevya, ugaidi, utakatishaji fedha.

Kati ya sababu zilizowasilishwa na Sanga wakati wa kufungua kesi hiyo ni pamoja na kudai kuwa uhuru binafsi na dhana ya kutokuwa na hatia ni haki ya kikatiba iliyohakikishwa Katiba ibara ya 13(6)(b) pamoja na ibara ya 15(1) na (2) 

Pia alidai Kifungu hicho kinachukua mamlaka ya mahakama ambayo ndiyo chombo chenye mamlaka ya kuamua haki za Watanzania ikiwa wana hatia au hawana kama ilivyoainishwa katika ibara ya 13(3). 

Sababu nyingine alidai ni kukiukwa kwa haki za  binadamu kunakopingana na mikataba ya kimataifa ikiwemo Azimio la Haki za Binadnu la mwaka 1948.

 Baada ya Mahakama ya Rufaa kusikiliza rufaa hiyo itapangwa tarehe ya hukumu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles