29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yaongeza siku tatu uandikishaji wapiga kura

TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo ameongeza siku tatu za kujiandikisha katika orodha la wapiga kura kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri Jafo, kupitia Ofisi ya Tamisemi imeeleza kuwa muda huo umeongezwa mpaka Oktoba 17, mwaka huu.

Pamoja na hali hiyo pia baadhi ya kata za jiji la Dar es Salaam wamelazimika kutumia magari ya matangazo  kuzunguka mitaani ili kuhamasisha wananchi kujiandikisha kupiga kura.

MTANZANIA lilipita katika mitaa mbalimbali ya jiji hilo na kukutana na magari hayo yaliyokuwa yakihamasisha watu kwenda kujiandikisha.

Katika Mtaa wa Sokoni Kata ya Tandale Manispaa ya Kinondoni, mwandishi alikutana na gari la matangazo likiwa sokoni hapo hapo likihamasisha kujitokea kujiandikisha.

Hata hivyo katika vituo vinne vya mtaa huo gazeti hili lilishuhudia mawakala na waandikishaji wakipiga soga kutokana na kukosekana watu wa kujiandikisha.

Mmoja wa mawakala hao kutoka Chama cha ACT, Bahati Shauri aliiomba serikali kuongeza siku za kujiandikisha ili kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kujitokeza.

“Tunaiomba serikali kama kuna uwezekano iongeze muda wa kujiandikisha kwa kuwa leo tumebakiwa na siku moja tu kesho(leo),” alisema Bahati.

Alisema kazi ya kuwahamasisha wananchi kujiandikisha imekuwa ngumu kutokana na wao kutoa sababu mbalimbali.

Alisema sababu kubwa inayotolewa na wananchi ni kudhani kujiandikisha lazima uwe na kitambulisho cha mpigakura kilichotolewa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

“Wengine wanasema hawawezi kupoteza muda wao kujiandikisha kwa kuwa viongozi wanaowachagua wanawageuka,” alisema Bahati.

Naye wakala wa CCM, Hassan Gogo alisema changamoto inayojitokeza ni wananchi kutokujua vituo wanavyotakiwa kujiandikisha.

“Kuna watu wengi wanafika kujiandikisha ambao si wa mtaa husika hivyo kutulazimu kuwaondoa na baadhi yao tukiwaelewesha wanatumia lugha si za kistaarabu,” alisema Gogo.

Aliongeza kuwapo kwa idadi ndogo ya wanaojiandikisha inatokana na uelewa mdogo wa wananchi ambapo wengine wanadai kuwa uchaguzi si mkubwa hivyo hawawezi kupoteza muda kwa ajili yake.

Alisema pamoja na gari la matangazo kupita mara kwa mara lakini watu wamekuwa wagumu kujitokeza kujiandikisha.

“Kama unavyoona hapa kulivyo, na gari la matangazo nadhani mmekutana nalo hapo mbele linazunguka lakini watu bado wagumu kujitokeza,” alisema Gogo.

Naye Msimamizi Msaidizi, Kata ya Sinza Raymond Mwanga alisema wameagiza gari litakalopita mitaani kuwahamasisha wapiga kura kwenda kujiandikisha.

“Tunasubiri hapa tumeagiza gari la matangazo liweze kuingia mitaani kuhamasisha kwa kata nzima ya Sinza,” alisema Mwanga.

Alisema pamoja na kuwa watu wanaendelea kujitokeza kidogo kidogo lakini bado nguvu zaidi ya kuhamasisha inahitajika.

“Ninyi nendeni kwanza mpaka jioni tujishapitisha gari mtakuja kuchukua takwimu huenda wakaongezeka baada ya kutangaza,” alisema Mwanga.

Katika kituo cha ofisi ya kata kilichopo mtaa wa Sinza D kilionekana kuandikisha idadi ndogo tu ya wapiga kura mpaka mwandishi anaondoka kituoni hapo hakukuwa na mwananchi hata mmoja aliyefika kujiandikisha.

Mwandikishaji  Rehema Mapunda alisema uandikishaji unaendelea vizuri japo idadi ndogo ndiyo wamejitokeza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles