Na Brighiter Masaki, Dar es Salaam
Wadau wa Haki za Watoto nchini wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuhuisha mchakato wa kuwarejesha shuleni wasichana wanaopata ujauzito na kufanya maboresho ya sheria ya ndoa ili wasichana waolewe wakiwa na umri wa kuanzia miaka 18 badala ya miaka 14.
Akizungumza mapema Juni 16, 2021 jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika wakati mashirika 13 nchini ya kutetea haki za watoto yalipofanya maadhimisho hayo Mkurugenzi wa Taasisi ya Msichana Initiative, Rebeca Gyumi, amesema Mashirika hayo yametoa mapendekezo sita kwa serikali ikiwemo suala la mtoto wa kike kurejeshwa shuleni baada ya ujauzito na kuboresha sheria ya ndoa.
“Katika kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika sisi kama taasisi zinazotetea haki za watoto na wasichana tunasema katika masuala yanayohusu makundi haya ni vema serikali kuangalia nini matakwa ya kundi hili na kuwafanya kuwa sehemu ya kutatua changamoto hizo.
“Kama wadau tutaendelea kutoa ushirikiano wetu kwa serikali ili kuhakikisha tunajenga jamii na taifa imara lenye kujali haki na ustawi wa watoto, hasa watoto wa kike.
“Juni 16 kila mwaka bara la Afrika huandhimisha siku ya Mtoto wa Afrika. Siku hii ilianzishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1991 kuwakumbuka na kutambua mchango wa watoto waliopoteza maisha katika mauaji ya watoto yaliyotokea Soweto nchini Afrika Kusini. Juni 16, 1976, wakati watoto walipoandamana dhidi ya elimu duni ya kibaguzi waliyopewa na serikali ya kibeberu na kuomba kufundishwa kwa lugha zao wenyewe,”amesema Rebecca ka kuongeza kuwa;
“Katika kuadhimisha siku hii sisi mashirika yanayoshughulikia masuala ya wasichana pamoja na wanawake vijana tumeungana ili kupaza sauti kwa serikali na wadau mbalimbali wanaoshughulikia masuala ya ustawi wa watoto.
“Wasichana kuchukua hatua stahiki katika kuboresha na kusimamia ulinzi na haki za wasichana kama kundi lililo katika hatari kubwa ya kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ambapo takribani asilimia 40 ya watu kati ya umri wa miaka 15-49 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia,” amesema Rebecca.
Amefafanua kuwa, siku ya mtoto wa Afrika kwa mwaka 2021, inaadhimishwa kwa kauli mbiu ya ajenda 2040 ‘Afrika tuitakayo kwa ustawi wa mtoto’, ambapo katika nchi yetu kauli mbiu hii imetoholewa na kuwa “Maendeleo endelevu 2030; Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto”.
Katika kusimamia dhima ya kauli mbiu hizi ambazo zimejikita kwenye kutathmini hali ya utekelezaji wa haki mbalimbali za mtoto, lakini pia mwitikio wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) katika kutekeleza maeneo 10 ya vipaumbele kwenye ajenda ya 2040 ili kusimamia haki na ustawi wa mtoto.
“Nchini Tanzania Sheria ya Mtoto na.21 ya mwaka 2009 imeainisha haki 5 muhimu kwa watoto ambapo moja ya haki hizo inaitaka serikali na wadau kuwalinda watoto dhidi ya ukatili,” amesema Rebecca..
Katika maadhimisho hayo yaliokutanisha pia Haki Elimu, Her Ability Foundation na Hope for Young Girls Mkurugenzi wa Bint Salha Foundation, Salha Azizi na Mkurugenzi wa Binti Makini, Janeth John wamezungumzia kuimarishwa kwa miundombinu ya shule ili kuwalinda watoto wa kike kutoa elimu ya afya ya uzazi huku wakionesha madhara ya mafunzo ya unyago.
“Wasichana wamekuwa wakifukuzwa shule kwa sababu ya kupata ujauzito kwa kufuata taratibu ambazo hazina nguvu ya sheria bali kupitia taratibu zilizozoeleka.
“Pamoja na serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya elimu kuzuia mimba za utotoni bado mtoto wa kike anakosa huduma saidizi pale anapopewa ujauzito na kuondolewa katika mfumo rasmi wa elimu.
“Licha ya hivi karibuni kuwapo kwa jitihada za serikali kutoa fursa kwa wasichana kuendelea na masomo kupitia mifumo mbadala kama MEMKWA bado mifumo hii haijengi usawa kwa kumlazimisha msichana kutumia mifumo mbadala, tofauti na inavyofanywa Zanzibar,” amesema Janeth.