31.7 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali yamwita ofisa WHO sakata la kuwapo ebola nchini

Andrew Msechu -Dar es salaam

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk. Damas Ndumbaro, amekutana na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Tigest Mengestu, ambaye amesema hawajatoa taarifa zozote kuhusu uwepo wa ugonjwa wa ebola nchini.

Mkutano huo baina ya Dk. Ndumbaro na Dk. Mengestu umethibitishwa na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas kupitia ukurasa wake maalumu wa Twitter, akieleza kuwa WHO imekanusha taarifa zilizokuwa zikisambaa kuhusu uwepo wa ebola nchini.

Dk. Abbas alisema katika mazungumzo hayo baina ya Dk. Mengestu na Dk. Ndumbaro jana, mwakilishi huyo alikiri kuwa WHO haina ushahidi wowote wa kuwepo ugonjwa wa ebola nchini.

“Serikali imemwita Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) hapa nchini kupata kwa kina hoja za shirika hilo zinazosambaa kupitia vyombo vya habari.

“Mwakilishi huyo amesisitiza kuwa WHO haijasema wala haina ushahidi wowote kuwa Tanzania kuna ebola na itashirikiana na Serikali.

“Aidha, katika mazungumzo hayo WHO imeafiki kuwa kama kuna mahitaji ya kupata taarifa zaidi kutoka Serikali ya Tanzania, lazima utaratibu ulioainishwa katika miongozo ya taasisi hiyo na ambayo imeridhiwa na Serikali ifuatwe kikamilifu,” alisema Dk. Abbas kupitia ukurasa wake wa Twitter.

Taarifa iliyotolewa kupitia ukurasa wa Twitter wa Wizara ya Mambo ya Nje, ilionyesha sehemu ya kipande kilichorekodiwa kikimkariri Dk. Mengestu akieleza kuwa WHO haihusiki na taarifa hizo.

“Kwanza ninapenda kutoa shukrani za dhati kwa ofisi yako kwa kutupa fursa hii ya kuja kuelezea kilichotokea wiki mbili zilizopita. Suala hili ni vyema kujengewa uelewa baina yetu kabla ya kutoa suluhu.

“Katika suala hili ni kwamba WHO haikusema kuwa kuna ebola, ninapenda kuelezea kilichotokea, ni kwamba taarifa hiyo haijatokea kwenye ofisi zetu kuu, wala katika ofisi zetu za kanda, wala kwenye ofisi zetu nchini. Suala hili linatakiwa liwe wazi kwetu kuwa hakuna ushahidi wa uwepo wa ebola hapa,” alisema Dk. Mengestu.

CHANZO CHA TAARIFA

Mwishoni mwa wiki iliyopita, baadhi ya vyombo vya habari (siyo MTANZANIA) vilitoa taarifa vikieleza kuwa WHO imetoa taarifa ya malalamiko ikieleza kwamba uwazi na kasi katika kukabiliana na virusi vya ugonjwa huo hatari ni muhimu katika kudhibiti mlipuko ambao tayari umetajwa kuwa janga la afya duniani.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa Jumamosi, Septemba 21, ilieleza kuwa WHO imeeleza kwamba kufuatia taarifa zisizokuwa rasmi kuhusu visa vya ugonjwa na jitihada zake kupata taarifa kutoka kwa idara husika Tanzania kuhusu hali nchini, hawajapokea data za kliniki, matokeo ya uchunguzi, mawasiliano na watu husika na hata matokeo ya uchunguzi wa maabara waliofanyiwa wagonjwa hao wanaoshukiwa.

Vilieleza kuwa WHO ilituma kundi la wataalamu kuchunguza kisa cha ugonjwa usiojulikana na ubalozi wa Marekani ulifuatilia hatua hiyo kwa kutoa tahadhari.

Hatua hiyo ilisababisha uvumi katika mitandao ya kijamii kwamba ugonjwa huo hatari umeingia nchini.

Serikali ya Tanzania ilifutilia mbali uvumi kwamba kuna visa vya ugonjwa wa ebola nchini.

Baada ya kuibuka kwa taarifa za uwepo wa ugonjwa huo wiki mbili zilizopita, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliwaambia wanahabari Septemba 14 kwamba hakuna kisa hata kimoja cha ebola kilichoripotiwa.

Alisema Serikali imejiandaa kukabiliana na mlipuko wowote wa ugonjwa na tayari imefanya majarabio ili kujua jinsi ilivyojiandaa huku ikiweka tayari vituo vya kuwatenga waathiriwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles